KIKOSI cha Azam FC leo kinatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma kucheza dhidi ya wenyeji wao Dodoma Jiji, katika mchezo wa raundi ya 13 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kama ikifanikiwa kushinda itaiengua Simba kileleni.
Azam iliyoshinda michezo sita mfululizo hadi sasa, imepania kuendeleza ubabe huo kwa kuifunga Dodoma Jiji na kukaa kileleni mwa msimamo na kuiacha Simba ambayo kwa sasa inaongoza ikiwa na pointi 28.
Ikiwa na pointi 27, iwapo itashinda itafikisha pointi 30, na kushinda mechi saba mfululizo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Rachid Taoussi, amesema ni mara ya kwanza kufika jijini Dodoma tangu aanze kuifundisha timu hiyo, lakini amekiandaa kikosi chake kwa ajili ya kuendeleza mlolongo wa ushindi kwenye michezo yake ya Ligi Kuu.
"Najua mechi haitokuwa rahisi, Dodoma Jiji ni timu ngumu na wanapambana, lakini nasi tunataka kuendeleza ushindi wetu, tuna morali na tuna wachezaji wazuri zaidi," alisema kocha huyo raia wa Morocco.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Azam FC, Thabit Zacharia, amesema wamefurahi kufika tena Dodoma, jiji ambalo wana historia nalo, kwani ndipo timu yao ilipopandia daraja na kuingia Ligi Kuu.
"Kikosi chetu kiko kamili, wachezaji wetu wote wapo fiti kwa ajili ya mchezo huu. Tumefurahi sana kuwa Dodoma kwa sababu ni sehemu muhimu sana kwetu, ni sehemu ambayo tulipandia daraja mwaka 2007, tukaanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/09 na mara zote tukija hapa tunakuwa kwenye wakati mzuri," alisema Thabit, maarufu kama Zaka Zakazi.
Tangu ilipolazimishwa suluhu dhidi ya Mashujaa FC, Septemba 29 mwaka huu, Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Azam ilianza kupata ushindi mfululizo hadi kufikia michezo sita kwa kuifunga Namungo bao 1-0, ikaishindilia Prisons mabao 2-0, ikaipa kipigo cha mabao 4-1, KenGold, kabla ya kuichapa Yanga bao 1-0, baada ya hapo ikaifunga Kagera Sugar bao 1-0, kabla ya juzi kushinda mabao 2-1, mechi ikichezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Dodoma, Moses Mpunga amesema wamejiandaa vyema na mchezo huo, ikiwemo kuipa kipigo Azam FC ili kutuma ujumbe kwa timu zingine kuwa Uwanja wa Jamhuri ni machinjioni.
"Katika mechi hii tunataka kutuma ujumbe kuwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma si sehemu salama kwa timu za Ligi Kuu zikija hapa, huu ni uwanja mgumu, kila mmoja anauogopa, ni machinjioni hapa, tumejiandaa vizuri," alisema Mpunga.
Dodoma Jiji imeshinda mechi zake nne kwenye uwanja huo, kati ya tano ilizocheza, ambapo imepoteza mechi moja tu dhidi ya Simba ikifungwa bao 1-0, mechi iliyochezwa, Septemba 29, mwaka huu.
Wakati Azam ikiingia uwanjani leo ikiwa kwenye nafasi ya pili kwa michezo 12 iliyocheza, Dodoma Jiji ipo nafasi ya tisa, ikiwa imeshacheza mechi 12, ikikusanya pointi 16.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED