Bodi ya Chai Tanzania (TBT) imeanza juhudi za kurejesha masoko ya chai yaliyopotea kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazowakumba wakulima wa chai kutokana na kukosa soko la uhakika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Beatrice Banzi, alieleza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa bodi kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi. Banzi aliyasema hayo baada ya kutembelewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Chai ya Omani, Khalfan Abdullah, inayomiliki chapa maarufu ya chai Mumtaz.
Banzi amebainisha kuwa kampuni hiyo, ambayo zamani ilikua ikinunua chai kutoka Tanzania lakini iliacha kutokana na sababu mbalimbali, imekubali kurejea na kununua tani 100 za chai kila mwezi, sawa na tani 1,200 kwa mwaka.
“Wamesema kwamba ifikapo Desemba 15 wataanza tena kununua chai kutoka Tanzania. Hii ni hatua kubwa kwa wakulima wa chai hasa wa Mponde, Lushoto mkoani Tanga, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa soko la uhakika,” amesema Banzi.
Banzi ameeleza kuwa bodi hiyo pia imeanza kufungua masoko mapya na kurejesha yale yaliyopotea, ikiwa ni sehemu ya malengo ya Bodi ya Chai, Wizara ya Kilimo, na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha changamoto ya soko la chai inatatuliwa.
“Mbali na Oman, tumeanza mazungumzo ya kurejesha soko la chai nchini Sudan. Hivi karibuni, tulikutana na Balozi wa Sudan hapa nchini kuzungumzia namna ya kupanua soko la chai katika nchi hiyo,” ameongeza Banzi.
Pia amebainisha kuwa mnunuzi mkubwa wa chai kutoka Japan anatarajiwa kuja nchini hivi karibuni kwa ajili ya kutembelea mashamba ya chai na kuona fursa za biashara na uwekezaji.
Banzi amefafanua kuwa serikali tayari imeagiza mashine za kuchakata chai, hatua inayolenga kuongeza thamani ya chai inayozalishwa nchini na kupunguza changamoto za soko kwa wakulima.
Aidha, amewataka viongozi wa kampuni, mashirika, na vyama vinavyojihusisha na chai kuendelea kuwatembelea wakulima ili kusikiliza na kutatua changamoto zao.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Bodi hiyo, Selemani Chilo, amesema kufufuka kwa soko la chai la Oman kutaiingizia Tanzania Dola za Kimarekani milioni 1.5 kwa mwaka, sawa na shilingi bilioni 3.9.
Chilo ameongeza kuwa Bodi ya Chai itaendelea kushirikiana na mabalozi wa nchi mbalimbali na kushiriki katika makongamano ya kimataifa ya biashara na uwekezaji ili kupanua masoko ya chai na kuongeza mapato kwa wakulima.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED