Wawekezaji waomba kuwekeza karakana za kisasa

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:44 PM Dec 01 2024
Mkurugenzi wa At The Wheel, Amin Lakhani.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa At The Wheel, Amin Lakhani.

SERIKALI imeombwa kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza karakana za kisasa za magari kutokana na kuokoa muda wa matengenezo ya vyombo hivyo vya usafiri.

Mkurugenzi wa At The Wheel, Amin Lakhani akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mitambo ya kisasa ya kunyayua magari, amesema teknolojia hiyo mpya itakuwa inatumika kuinua magari badala ya kutumia kamba na itawasaidia mafundi kukamilisha matengenezo kwa wakati.

Amesema hivi sasa teknolojia duniani zinazidi kukua hivyo wao kama wawekezaji watazidi kupanua wigo wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kupunguza adha ya mafundi kutumia muda mrefu kwa ajili ya kufanya matengenezo ya gari ambalo limepata hitilafu barabarani.

Naye, Fundi wa magari, Ali Kawego amesema uwekezaji wa mitambo hiyo ya kisasa itawavutia vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ili kupata elimu ambayo itawasaidia kujiajiri wao wenyewe ili kujiinua kiuchumi.