WATU 700 wamepatiwa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika maonesho ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika jijini Arusha.
Huduma hizo zilitolewa kwa muda wa siku saba katika viwanja vya TBA Kaloleni, kutoka kwa wataalamu wanawake wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto na Mkuu wa Kitengo cha Utoaji wa Huduma Bora wa JKCI, Dk. Naiz Majani, alisema upimaji huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya wanawake, wajawazito na watoto, pia waliwahudumia na wanaume waliohitaji kufanyiwa uchunguzi wa moyo.
Dk. Naiz alisema wamefanya upimaji wa kipimo cha Echo, cha moyo kwa mtoto aliyepo tumboni kwa wajawazito 189 na saba kati yao walionekana kuwa na shida ya moyo.
“Tumefanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa watoto 114 kati ya hao tisa tumewagundua kuwa na magonjwa ya moyo ya ambayo ni matundu, mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake na shida za valvu za moyo tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”.
“Ninatoa wito kwa wazazi kuwaleta watoto wao kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo pale zinapotokea nafasi za upimaji kama huu tulioufanya Arusha kwani magonjwa mengi ya moyo kwa watoto kama yatagundulika mapema watoto wanatibiwa na kupona kabisa,” alisema Dk. Naiz.
Alisema watu wazima waliowapima walikuwa 397 wanaume wakiwa 99 kati ya hao 397 waliopewa rufani ya kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupata matibabu ya kibingwa katika taasisi yao iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam walikuwa 19.
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo JKCI, Dk. Engerasia Kifai, alisema magonjwa ya moyo waliyokutwa nayo watu wazima yalikuwa ni shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa vyumba vya moyo, makovu kwenye valvu za moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo.
Pia, hitilafu kwenye mfumo wa umeme wa moyo na magonjwa ya kuzaliwa kama vile tundu kwenye moyo huyu alikuwa mgojwa mmoja.
Dk. Kifai alivitaja visababishi vya magonjwa wa moyo kwa watu wazima kuwa ni uzito mkubwa, utumiaji wa vilevi kuzidi kiwango kinachotakiwa, utumiaji wa tumbaku, utumiaji wa chumvi zaidi ya kiwango kinachotakiwa, kuwa na kiwango kikubwa cha lehamu kwenye damu.
Kadhalika, kutokufanya mazoezi, kuwa na shinikizo la juu la damu, kuwa na ugonjwa wa kisukari, kuwapo na magonjwa ya moyo kwenye familia, kutokula mlo kamili, kupumzika muda kidogo au kutopata muda wa kutosha wa kupumzika na msongo wa mawazo
“Baadhi ya dalili za magojwa ya moyo kwa watu wazima ni kuumwa kwa kifua mara nyingi huambatana na uzito ama mgandamizo wa kifua, kupungukiwa na pumzi, kukohoa, kuchoka bila sababu, mapigo ya moyo kwenda haraka haraka au mapigo ya moyo kutokupiga kwa mpangilio au kuwa chini ya kiwango ikiambatana na kuchoka sana ama kudondoka na kupoteza fahamu na uvimba kwa miguu ambapo hubonyea ukiikandamiza,” alisema Dk. Kifai.
Alisema ili kuepukana na magonjwa ya moyo ni muhimu kwa watu wakafuata mtindo bora wa maisha, ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula chakula bora, kutotumia bidhaa aina ya tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza na kujenga tabia ya kupima afya japo mara moja kwa mwaka.
Lemaiya Laizer, mkazi wa Loliondo, ambaye mtoto wake alifanyiwa uchunguzi na kugundulikwa kuwa na tatizo la tundu kwenye moyo, alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema kuwa imempunguzia safari ya kwenda KCMC kufanyiwa vipimo vya moyo na kupata matibabu.
“Mwanangu anashida akicheza kidogo anachoka pia ukuaji wake ni tofauti na watoto wengine, nikiwa Loliondo niliandikiwa rufaa ya kwenda KCMC, baada ya kusikia kuna wataalamu wa moyo hapa nimemleta mwanangu ambaye amepima na kukutwa na shida na nimepewa rufaa ya kwenda Dar es salaam ili akapate matibabu ya kuzibwa tundu hilo,” alisema Laizer.
“Baada ya kusikia upimaji wa moyo unafanyika hapa kwa wanawake na watoto niliona nije kujaribu bahati yangu kwani mimi ni mwanaume na kuna wakati moyo wangu unakwenda kasi sana na ninashindwa kulala vizuri hasa usiku.
“Namshukuru Mungu nimefika hapa hawajanifukuza na nimepata huduma ya vipimo, ushauri na matibabu ya moyo na sijalipia chochote,” alishukuru Mohamed Juma mkazi wa Sanawari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED