MTAALAMU wa Uchumi na Mkufuzi wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT), Dk. Isaac Safari amesema kupaa kwa dola ni taarifa ya tahadhari kwa nchi kuwa iongeze uzalishaji wenye tija ili kukuza thamani ya shilingi.
Akizungumza na Nipashe Digital kwenye mahojiano kuhusu kupaa kwa Dola ya Marekani, Dk.Safari amesema kuzidi kupanda kwa thamani ya dola kunatafsiri mbili ambazo ni pamoja na mahitaji yake kwa watumia wa shilingi kuongezeka huku upatikanaji wake kama sarafu ya kimataifa ukipungua nchini.
“Ukichanganya vyote hivyo viwili shilingi itaonekana dhaifu kuliko dola kwani dola itaonekana kuwa bora zaidi kutokana na uhitaji wake.
“Athari yake ni kubwa sana kutokana na kuwa italilazimu Taifa kutumia nguvu ya ziada hata kwa kuingia mfukoni zaidi kwa maana ya benki kuu kutafuta dola za kutosha kwaajili ya wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje ya nchi,”amesema Dk. Safari.
Aidha, amesema chanzo cha hali hiyo ni kupungua kwa uwekezaji kutoka nje, kupungua kwa misaada iliyokuwa ikileta fedha za kigeni nchini, ikiwemo dola ya marekani na kuwa ni jukumu la Benki Kuu Tanzania (BoT) kutafuta namna ya kuongeza fedha hiyo nchini.
Amesema wafanyabiashara wanahitaji kuagiza vitu muhimu kama vipuli, magari pamoja na vifaa vingine muhimu ambavyo havizalishi nchini na kuwa vyote vinahitaji dola ya marekani hivyo hali itazidi kuwa ngumu na kusababisha kupanda kwa bidhaa za nje.
MAFUTA KUPAA BEI
Kwa mujibu wa Dk. Safari, kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol, dizeli pamoja na mafuta ya taa tangu Januari ni kiashiria tosha juu ya ukosefu wa dola nchini.
“Lakini uuzaji wa mafuta unategemea ni kiasi gani cha mafuta yanayoletwa nchini, lakini kama waagizaji hawana dola lazima tutaona atahri ya kupanda kwake kwani hatuna dala ya kutosha ya kuagiza mafuta,”amesema Dk.Safari.
Aidha, amesema tatizo linguine ni maamuzi binafsi ya Rais wa Marekani, Donald Trump akitaka Taifa hilo liendelee kuwa na nguvu na kuheshimika zaidi akihusianisha na suala lake la kunesha nia ya kutokutoa fedha kufadhili vita pamoja na kukataa biasharra isiyokuwa na faida kwa taifa hilo.
“Kwa upande mwingine anaweza kuwa anazuia dola kutoka ili kulinda uchumi wa nchi yake kwani uchumia wa marekani ni sarafu vilevile kwahiyo suala hilo linaweza kuathiri nchi nyingi duianiani na si Tanzania na shilingi yake pekee,”amesema Dk.Safari.
SULUHISHO
Amesema jambo la kuzingatia kwa sasa ni kuongeza uzalisha wenye tija wa bidhaa za ndani ili ziuzwe nje na kuleta fedha ya kigeni, vilevile kuendelea kuwashawishi watanzania waishio nje kuhakikisha wanafanya uwekezaji wa nguvu na kuleta fedha za kigeni.
“Sisi Tanzania tufanye nini ili uchumi wetu ubaki na nguvu uendelee kuimarika ni kufanya uzalisha na kuongeza tija ya bidhaa za watanzania wenyewe,”
“Kweli wageni watakuja kuzalisha ndani lakini mwisho wa siku wataondoka na faida ambayo siyo Shilingi ya Tanzania kwahiyo kwa njia hiyo dola itazidi kupungua nchini hivyo tuanze sisi wenyewe,” amesema Dk.Safari.
Aidha, alisema uwekezaji mkubwa uendelee katika mabadiliko ya kielimu ili kuwaongezea watanzania ubunifu wa kufanya uzailisha na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani ikiwemo za kilimo.
“Mwisho wa siku mambo mengi tukizalisha wenyewe ikiwemo vifaa vya ukarabati wa vyombo vya moto ambavyo hatuna maana ya kuendelea kutegemea kutoka nje pengine ikifikia mahali tuanze kuzalisha magari sisi wenyewe,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED