RIPOTI MAALUM - 1 Mfumo dume , ndoa ya mitala ulivyozima ndoto ya mhasibu

By Neema Emmanuel , Nipashe Jumapili
Published at 05:47 PM Jun 30 2025
Mwandishi wa habari wa gazeti hili, Neema Emmanuel (kulia), akifanya mahojiano na Mary Mashauri, mkazi wa Ihayabuyaga, hivi 
karibuni.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwandishi wa habari wa gazeti hili, Neema Emmanuel (kulia), akifanya mahojiano na Mary Mashauri, mkazi wa Ihayabuyaga, hivi karibuni.

WAKATI mwanamke anapambana kufanya kazi kumsaidia kiuchumi mwenza wake ili kupingana na kauli ya ‘golikipa’kusubiri kila mpira adake, hali hiyo ni tofauti katika familia ya Mzee Marko Kanyeji.

Kwake si ruhusa mke wake yeyote kufanya kazi ya kujiingizia kipato, bali ni jukumu lao kukaa nyumbani kulea watoto sambamba na kujishughulisha na kilimo ili kupata chakula nyumbani.

Ni Jumapili iliyojaa utulivu na mawingu kiasi yakiambatana na kibaridi ambacho si lazima kukivalia sweta, ambapo safari ya takribani kilometa 26 kwenda katika Kijiji cha Ihayabuyaga, Magu mkoani Mwanza inaanza.

Baada ya kufika mwandishi wa habari hii anapokewa na Mary Mashauri (33), ambaye ni mmoja wa wake wanane wa Mzee Kanyeji. Mary ni msomi mwenye Astashahada ya Uhasibu ambayo mazingira yamechangia afungie kabatini taaluma yake, akitegemea Sh. 3,000 kwa siku ya matumizi ya nyumbani anayopewa na mume wake kulingana na hali itakavyokuwa.

Mary ni mama wa watoto wanne, wa kwanza akiwa na umri wa miaka 10 na wa mwisho miaka miwili ambao kati yao wa kike ni wawili.

Wanaishi katika nyumba yenye vyumba viwili vya kulala na sebule aliyopangi wa na mume wake, mfanyabiashara wa samaki.

SAFARI KIELIMU
Mary anasema alisoma katika Shule ya Msingi Nangwa, Hanang’ mkoani Manyara kati ya mwaka 2000 na 2007 na kujiunga Shule ya Sekondari Hanang’ akisoma kati ya mwaka 2008 na 2011, na mwaka 2012-2015 aliposomea uhasibu.

Anasema baada ya kuhitimu alipata kazi katika moja ya taasisi za kifedha na kufanya takribani miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 na baadaye kuolewa.

 Anasema aliacha kazi baada ya mume wake kumwahidi kumfungulia biashara, ahadi ambayo hadi sasa haijatimizwa.

Mary anatafsiri hali hiyo na mengi yaliyomtokea kuwa ya na changiwa na mfumo dume ambao anaona umebadili maisha yake. 

Kwa sasa hawezi kufanya jambo lolote bila ya kumshirikisha mumewe.

Anasema endapo atafanya jambo bila kuomba ridhaa ya mume wake, huingia katika mgogoro na familia. 

“Hali hii imeniathiri katika mpangilio mzima wa maisha yangu kuanzia kiuchumi, kifikra na hata kiutendaji. Hadi sasa sielewi muhstakabali wa maisha yangu. Kila kukicha mambo ni yale yale,” anasema huku akibainisha kuwa kabla hajaolewa alikuwa na hali nzuri kiuchumi, alikuwa amewekeza vitu mbalimbali lakini baada ya kuolewa vimesimama.

“Kwa sasa hakuna kazi ni nayoifanya zaidi ya kilimo kwa ajili ya chakula cha nyumbani. Msimu wa kilimo ukimalizika, huwa ninakaa nyumbani. Ninajua kabisa jamii imekosa ushiriki wangu wa kutoa huduma kwao. Licha ya kuwa na elimu, nimekuwa mama wa nyumbani.”anasimulia.

USHAURI KWA VIJANA
Mary anawashauri vijana hasa wanaotoka vyuoni kabla ya kuingia kwenye uhusiano ni vyema wakapata elimu ya uhusiano ili kujiepusha na mfumo dume. 

Pia anaziomba taasisi zinazohusika na utetezi wa haki za wanawake kufika maeneo ya vijijini ili kuwanusuru wanawake wanaonyanyaswa na mfumo dume.

Taasisi ya Equality for Growth (EfG) inatafsiri ukatili kuwa ni kitendo chochote kinachoweza kumsababishia mtu mwingine madhara ya kimwili, kiakili au kisaikolojia sambamba na vitendo vyenye kusudio la kulazimisha au kutisha mtu na kusababisha anafanya jambo kinyume na matakwa yake.

Hatua ya Mary kuzuiwa kushiriki katika shughuli za kujiingizia kipato kupitia taaluma yake, huku akisalia kuwa mama wa nyumbani katika hali duni, inatajwa kuwa sehemu ya ukatili wa kijinsia.

Licha ya Tanzania kuwa moja ya nchi zilizoridhia mikataba mbalimbali kuhusiana na ukatili wa kijinsia ikiwamo Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948; Mkataba Mwingine ni Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake ( C E D A W ) wa 1979Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika (Maputo Protocal) wa mwaka 2003 na Azimio la Beijing la Masuala ya Jinsia la 1995, bado ukatili katika nyanja mbalimbali umekithiri.

MUME AJITETEA
Akizungumza na Nipashe kuhusu kumwachisha mkewe kazi kwa ahadi ya kumfungulia biashara, Mzee Kanyeji anasema hiyo ilikuwa nia yake lakini kuyumba kwa biashara zake kumechangia kutoitimiza ahadi hiyo.

“Sioni sababu ya mke kulalamika kwani kukaa na familia nalo ni jukumu. Kuhusu suala la kumfungulia biashara si kwamba limeishia hapo. bado ninajipanga ili naye ajiwezeshe kiuchumi ili kumudu mahitaji yake madogo madogo. Ninampenda mke wangu. Ninachokipata ndicho ninakigawa kwa familia zangu,” anasema.

ALAZIMISHWA KUOLEWA
Aisha Ahmed (si jina halisi) ambaye pia ni mwathirika wa ukatili wa kijinsia,anasema manyanyaso dhidi ya wanawake ni makubw akitolea mfano jamii za wafugaji alikoz aliwa.

Anasema katika jamii hiyo mwenye sauti na uamuzi ni baba na akiwa hayupo, mjomba au ndugu yeyote wa kiume ndiye anaongoza familia.

Anasema baada ya kuhitimu kidato cha nne, akiwa na ndoto ya kujiendeleza kielimu, alizuiwa kuendelea na masomo na kulazmishwa kuolewa.

“Nilitoroka nyumbani na kukimbia zaidi ya nusu saa katikati ya msitu wa kutisha na giza nene. Sikuogopa tembo wala wanyama wakali. Nilifanya uamuzi mgumu, sikuhitaji kukandamizwa bali nilihitaji kusoma,” anasema.

Kwa sasa, anasema anaendelea vyema katika kituo cha malezi kwa mabinti waliathiriwa na ndoa za utotoni katika Chuo cha Biblia cha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Nyakato, jijini Mwanza.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.
WAHOFIA VISHAWISHI
Mussa Ghalani, baba wa watoto wawili, anasema mke wake hubaki nyumbani kuangalia familia akiamini kumpa nafasi ya kufanya biashara au kuajiriwa anaweza kumpoteza. 

Anasema huko mtaani anaweza kukutana na vishawishi vitakavyochangia kuleta mifarakano nyumbani.

“Ukitaka kumpoteza mkeo mruhusu kufanya kazi. Kwanza, wanawake wengi wakifanya kazi wanaanza kuwa na dharau. Hata majukumu yake ya msingi kuna wakati anashindwa kuyatimiza akisingizia amechoka,” anadai.

Kauli hiyo ya Ghalani inapigwa vikali na Violeti Chenga, mkazi wa Kijiji cha Isangijo, wilayani Magu, anayesema mwanamke akipewa nafasi anaweza kutekeleza majukumu yote bila tatizo.

UKATILI KISIASA
Mkazi wa Kisesa, wilayani Magu, Moze Kapaya, anasema mara kwa mara amekuwa akishuhudia matukio ya unyanyasaji ambao mengi hufanyika kwa kificho.

Kipaya anatoa mfano wa binti aliyekuwa akiwania nafasi ya kisiasa, ambaye alibaguliwa na kutukanwa na baadhi ya wanaume kwa kuangalia jinsia yake kwa kisingizio cha utamaduni ya jamii anayotoka.

“Nafasi ya kupinga mila kandamizi ipo endapo tutaanza kuelimisha jamii kupitia mitandao na vyombo vya habari,” anasema huku akishauri elimu ya kijinsia ianze mapema shuleni na nyumbani na wazazi wabadili njia ya malezi ya watoto kwa kuweka usawa.

Pia anasema sera na sharia zitekelezwe kikamilifu kuhakikisha wanawake na wanaume wanakuwa na fursa sawa.

KAULI YA SERIKALI
Mtendaji wa Kijiji cha Ihayabuyaga, Revocatus Mtesigwa, anakiri kuwapo kwa mfumo dume katika eneo lake, akieleza kuwa sehemu kubwa huhusisha wanawake na watoto kutokushirikishwa katika mambo ya maendeleo.

“Hata tukiitisha vikao vya kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, uamuzi hufanywa na wazee wa kiume au viongozi wanaume pekee, hata kama wanawake na vijana ndio wanapokea athari kubwa za miradi hiyo,” anasema.

Anasema katika eneo hilo na maeneo jirani, wanawake wengi huonekana kama wasaidizi tu na kuwa hawapewi fursa za kiuongozi kusaidia.

Anahusisha hali hiyo na mila na desturi za jamii hiyo ambazo wanawake hata kumiliki ardhi au kushiriki kwenye baadhi ya shughuli, hasa zinazohusisha fedha au uamuzi hawawezi.

“Ofisi yangu inatumia mbinu mbalimbali zenye lengo la kuelimisha, kushirikisha, na kubadilisha mitazamo ikiwamo elimu na uhamasishaji programu za malezi bora na kuongeza kwa uelewa kuhusu usawa wa kijinsia,” anasema.

Mtesigwa anataja athari za mfumo dume katika jamii yake kuwa ni pamoja na kukosekana kwa uamuzi wa pamoja katika  familia, watoto wa kike kunyimwa fursa za elimu, kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia, unyanyasaji wa wanawake na watoto wa kike majumbani pamoja na kukithiri kwa ndoa za utotoni.

HALI YA UKATILI
Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za unyanyasaji na ukatili wa kijinsia 2022-2023 nchini iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, waathirika 37,448 wanaoishi Tanzania, walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji.

Kwa mwaka 2023, waathirika wengi walikuwa wanawake 25,420 sawa na asilimia 67.9  na wanaume walikuwa 12,028 ambao ni asilimia 32.1.

Waathirika waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wameongezeka kwa asilimia 22.5 kutoka 30,566 mwaka 2022 hadi 37,448 mwaka 2023.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa idadi ya wanaume imeongezeka kwa asilimia 32.2 kutoka waathirika 9,100 mwaka 2022 hadi 12,028 mwaka 2023, na wanawake wameongezeka kwa asilimia 18.4 kutoka 21,466 mwaka 2022 hadi 25,420 mwaka 2023.

Kutokana na takwimu za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia zilizobainishwa, NBS inashauri juhudi zifanyike kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kwa kuwa ni vitendo ambavyo vinaweza kupunguza nguvu kazi ya taifa na kuacha familia na waathirika katika hali ya sonona na umasikini.