“SIKUJUA kama nitakuwa mhanga (mwathirika) wa kiharusi.” Alisikika mgonjwa mwenye miaka 45 mwenye familia ya watoto wawili na mume aliyepata ahueni na kuweza kuongea kidogo huku akiwa hawezi kutembea kabisa katika kitengo cha dharura usiku wa manane.
Imeandikwa Na Dk. Mabula Budodi
“Nilikuwa nadhania kiharusi kinawapata watu wazee tu wenye umri kuanzia miaka 60 na zaidi. Nilivyokuwa napima mara nyingi na kukutwa na tatizo la shinikizo la damu, madaktari walinishauri kuanza kutumia dawa za kushusha shinikizo la damu na kubadilisha mfumo wangu wa maisha lakini sikutaka hata kusikia.
Ni kama wiki moja kabla ya kupata tatizo hili, alisema alianza kujisikia ovyo ovyo kwa kuanza kupata maumivu makali sana ya kichwa yasiyopoa hata kwa dawa ya kichwa, pia alianza kuona kizungu zungu kikali na hata kutokuona vizuri, yani uhafifu wa kuona uliongezeka siku baada ya siku bila ya kujua sababu ni nini.
Kutoana na hali hiyo, anasema aliishia tu kwenda dukani kununua dawa ya malaria na kuanza kutumia lakini kichwa kiliendelea kuuma sana.
Alishia kusema anajuta kutokufuata ushauri wa daktari na hakika anajuta maana hata kutembea na uwezo wa kwenda kazini hana kwa sasa.
“Nina uhakika kama nilijua inaweza kuwa kwa namna hii, ningetumia dawa vizuri sana,” alisema kwa masikitiko makubwa.
Kiharusi ni ugonjwa wa dharura ambao hutokea baada ya ubongo kukosa damu na kwa muda.
Ubongo wa binadamu unahitaji damu na okisijeni ili kufanya kazi zake za kila siku kisawia. Kama ikitokea ubongo umekosa kupata damu kwa mda mfupi mpaka muda mwingi, unaweza kuleta madhara makubwa kama kushindwa kutembea, kuongea na hata kufanya shughuli za kila siku.
Kiharusi kimekuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakumba watu hasa wenye matatizo la shinikizo la damu, kuwa na tatizo la ugonjwa wa kisukari, tatizo la kuwa na lehemu (corestoral) nyingi katika mishipa yako ya damu ambayo huweza kusabababisha kuziba kwa mishipa hiyo na kufanya ubongo kukosa damu na okisijeni. Kuvuta sigara husababisha kuharibika kwa mishipa ya damu ha hata pia kunywa pombe kwa kupitiliza.
AINA ZA KIHARUSI
Kuna aina mbili mpaka tatu za kiharusi, yaani kiharusi kinachosababishwa na damu kuvujia au kuvilia kwenye mishipa ya ubongo na damu kugandia kwenye mishipa ya ubongo. Pia kuna kiharusi cha kupita ambacho mtu anaweza kupata madhara ya muda tu ambayo huweza kurudi katika hali ya kawaida ndani ya saa 24.
Pamoja na kuwa na aina hizi za kiharusi zote bado huweza kuishia katika madhara makubwa kama yatajwayo hapo mwanzo, matababu yake huchukua muda mrefu sana na unahitaji watalamu tofauti tofauti ili kusaidia kupata haueni kidogo ya kutembea hata kuongea kwa kueleweka. Ni mara chache sana kurudi kuwa na hali uliyokuwa nayo mwanzo kabla ya kupata kiharusi.
Kwa hiyo matubabu yake inahitaji kada tofauti tofauti kama watu wa mazoezi ya viungo, mazoezi ya kuongea na matumizi ya dawa pia.
Ukweli ni kwamba tatizo la kiharusi linaweza kuzuilika kwa kuangalia afya yako, kufatilia na kufuata ushauri wa dakitari, matumizi mazuri ya dawa za sukari, shinikizo la damu, kutokunywa pombe kupita kiasi au kuvuta sigara.
Ni vyema kukinga kuliko kutibu maana mwisho wa siku husababisha kuishia kwenye ulemavu wa kudumu na kupoteza nguvu kazi katika jamii hata familia kwa ujumla hasa pale anapopata mtu ambaye ni nguzo na mhimili mkuu kakika familia.
· Dk. Budodi ni daktari wa magonjwa ya binadamu na anaishi Dar es Salaam. Kwa ushauri anapatikana kwa simu 0710 980096 na barua pepe mabulabudodi@gmail.com
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED