“HIYO siku naikumbuka sana. Ni kama jana tu kwangu maana donda lilianza kama utani. Kilianza kimchubuko kidogo ambacho kilisababishwa na kujikwaa kwenye kimti mguuni. Hata sikuchukulia maanani maana nilijua itakuwa kama siku zote ni kimchubuko cha kawaida kitapona ndani ya siku moja au mbili, hivyo maisha yakaendelea kama siku zote.
“Lakini haikuwa hivyo baada ya siku ya kwanza, niliona dalili ya kuanza kupona, lakini kadiri siku zilivyoenda kilianza kutoa maji maji na kuanza kuchimbika. Nilishangaa na kujiuliza maswali mengi kwa nini inakuwa hivi?
“Nilijijibu moyoni tu labda kwa sababu sikupata kuchoma sindano ya tetanasi ndiyo mana kimekuwa kikubwa. Nilikwenda zahanati na kuomba kuchoma sindano ya tetanasi na kisha kusafisha kidonda na kuondoka huku nikiwa na matumaini makubwa kwamba sasa nitakuwa salama.”
Hiyo ni kauli ya mgonjwa ambaye alipata tatizo ambalo hakujua chanzo ni nini. Anasema tokea hapo aliona dalili ya ongezeko la kidonda hicho. Hali hiyo, anasema ilianza kumfanya awaze kweli na hata kuanza kuhisi vitu vingi kichwani.
Anasema kadiri muda ulivyosonga, aliona hali ikiendelea hivyo na siku moja alikutana na rafiki yake amabaye ana kisukari na kumshauri kwamba anasema labda anaweza kuwa na tatizo la sukari, hivyo inabidi akapime. Alimkatalia na kusema kwao hakuna suala la sukari. Aliendelea kusafisha kidonda na kutumia dawa za kienyeji kwenye kutibu kidonda.
“Ni kwa namna gani nilikuwa na uelewa mdogo sana kuhusu ugonjwa wa sukari, kadiri siku zilivyoendelea sikupata ahueni hata kidogo zaidi ya kuendelea kuoza mguu kutokana na janga hilo. Niliogopa kweli na kujiuliza tena maswali mengi yasiyo na majibu kichwani.
“Niliamua kufuata ushauri wa rafiki yangu aliyenishauri siku nyingi zilizopita na kutembelea hospitali, tena hospitali kubwa. Nilikutana na daktari aliyenisikiliza na kuniuliza maswali kadhaa mojawapo likiwa huwa nina matatizo ya sukari na nilishawahi kupima. Nilijibu kwa hofu kuwa hapana sijawahi kupima sukari.
“Nilijawa hofu maana nilishasikia taarifa nyingi za watu wa sukari kuhusu kutokula vyakula karibia vyote ninavyovipenda na kunywa dawa nyingi zisizo na hesabu, anabainisha.
Baada ya maelezo hayo, anasema daktari alimwambia kuwa kama alivyomweleza kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na tatizo la sukari, hivyo wanaweza kupima kiwango cha sukari kwa wakati huo, sukari ya kufunga bila kula chakula ndani ya saa nane na kiwango cha sukari ya ndani ya miezi mitatu ili kupata uhalisia zaidi juu ya kiwango cha tatizo.
Baada ya majibu kutoka aliambiwa sukari na inasoma iko 28 kwenye kipimo na inaashiria kwamba miezi mitatu isomeke 13 na wanatarajia iwe chini ya 6.5% kwa mtu ambae hana matatizo ya sukari.
“Hivyo kama ukiwa unasukari ya kiwango cha kawaida inayotakiwa itasaidia kwenye kupona kwa kidonda hicho. Akasema sasa tutaanza matibabu, nitakuelekeza namna ya kuishi na sukari,” anasimulia.
Anasema masharti na maelekezo aliyopewa hayakuwa magumu kufuata si kama alivyokuwa anasikia kwa watu wa mtaani na vitisho kuhusu sukari. Ndani ya miezi miwili mpaka mitatu kidonda kilikuwa kimepona kabisa na aliendelea na maisha mengine kama kawaida huku akihudhuria kiliniki ya sukari kila mwezi bila kuacha.
HALI DUNIANI
Inakadiriwa kuwa watu milioni 422 wanaishi na ugonjwa wa kisukari duniani kote, ikiwa ni mara nne zaidi ya miaka 40 iliyopita kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kisukari ni ugonjwa unaoelezewa na kuwa na kiwango kikubwa cha sukari mwilini kwa sababu ya mwili kutokutumia insulini vizuri au kutokuzalisha insulini ya kumeng’enya sukari mwilini.
Kuna aina kuu mbili za kisukari. Kisukari aina ya kwanza ambacho hupatikana kwa Watoto na vijana huanzia umri mdogo na husababishwa zaidi na mwili kutokuzalisha insulini ya kutosha.
Sukari ya aina ya pili huanza katika umri mkubwa, yaani kwa watu wazima na husababishwa na mwili kutokutumia insulini iliyoko mwilini.
Dalili za ugonjwa wa kisukari mwilini ni kukojoa mara kwa mara bila hata kunywa maji, kiu iliyopitiliza hata mtu akitaka kunywa maji muda si mwingi, kupungua uzito bila sababu isiyoeleweka, kuwa na njaa iliyopitiliza hata baada ya kula mda mfupi, kuchoka sana mwili, kutokuona vizuri, kutokupona vidonda mapema na hata pia kuumwa mara kwa mara.
MATIBABU YAKE
Matibabu ya kisukari huhusisha kubadili mfumo wa maisha na matumizi ya dawa, yaani kufanya mazoezi, kupima sukari mara kwa mara, kula vizuri majani na mboga zaidi na kupunguza wanga na kupunguza msongo wa mawazo.
Madhara ya sukari huweza kutokea kwenye moyo, figo, macho na hata kutokuweza kuhudumia familia kwa wanaume na hata mwili mzima kudhoofika. Jambo la msingi ni kuzingatia matibabu, kufuatilia afya kwa kupima hasa kwa mtu ambaye hajagundulika na kuwa na tatizo la sukari.
Ni muhimu kufuata masharti na ushauri wa daktari.
· Dk. Budodi ni daktari wa tiba ya binadamu anapatikana kwa simu namba 0710 980096 na baruapepe mabulabudodi@gmail.com
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED