Wakala wa Nishati Vijijiji (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza uoto wa asili nchini pamoja na kulinda barafu katika Mlima Kilimanjaro.
Rai hiyo imetolewa Disemba 10 na Afisa kutoka REA, Praygod Ng’unda mara baada ya kushuka kutoka Kilele cha Uhuru katika Mlima Kilimanjaro akiwa ameambatana na Afisa Rasilimali Watu na Utawala kutoka REA, Tecla Nyerere walioshiriki hafla ya kusherehekea miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kupanda Mlima huo.
Kampeni hiyo inayoongozwa na Hifadhi za Taifa (TANAPA) iliyopewa jina la Twenzetu Kileleni Msimu wa 4 yenye kauli mbiu ya stawisha uoto wa asili Tanzania, okoa barafu ya Mlima Kilimanjaro ilianza Disemba 3, 2024.
“Sisi kama REA tunaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi wa kupikia barani Afrika na Duniani kwa ujumla. Tumeanza kutoa majiko ya gesi na majiko banifu kwa bei ya ruzuku ili kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Tumeshiriki kampeni ya mwaka huu ya kusherehekea miaka 63 ya Uhuru wa nchi yetu kwa kupanda Mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza vivutio vyetu mbalimbali vya utalii tulivyo navyo pamoja na kulinda barafu katika Mlima Kilimanjaro kama ilivyo kauli mbiu ya kampeni ya mwaka huu,” amesema Ng’unda.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED