SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973, ambao pamoja na mambo mengine, utaweka sharti la kuvaa kofia ngumu abiria na dereva wa bodaboda.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Asha Abdallah Juma.
Asha alihoji lini serikali itakuja na kipengele kwenye Sheria ya Usalama Barabarani cha kulazimisha uvaaji wa kofia ngumu kwa abiria na madereva wa bodaboda.
Sillo akijibu swali hilo, alisema sheria iliyopo sasa ina upungufu na hailazimishi abiria kuvaa kofia ngumu na kumhakikishia mbunge huyo kuwa katika maboresho ya sasa ya sheria hiyo jambo hilo limezingatiwa na sasa itakuwa ni lazima kuvaa kofia ngumu kwa abiria na dereva wa bodaboda.
Katika swali la msingi, Mbunge Viti maalum (CCM), Amina Ali Mzee, alihoji lini serikali itaanza kuweka sheria na uratibu mzuri wa kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na uzembe wa madereva.
Akijibu swali hilo, Sillo alisema Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama Barabarani kwa sasa inasimamia masuala ya usalama barabarani kwa kutumia Sheria ya Usalama barabarani Sura 168 ya mwaka 1973 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2002.
“Katika mkakati wa kuboresha sheria hii ili kupunguza ajali za barabarani serikali imekusanya maoni kutoka kwa wadau na sasa inamalizia kuyafanyia kazi na baada ya hapo itawasilisha muswada wa sheria bungeni,” alisema.
Katika swali la nyongeza, alihoji hatua zipi zinachukuliwa na serikali kuwadhibiti madereva wazembe na serikali na haioni kuna haja ya sheria hiyo kuja bungeni ili kudhibiti ajali za barabarani.
Naibu Waziri Sillo, alisema serikali inachukua hatua kwa madereva wazembe kwa kuwafutia leseni na hufikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zingine kisheria.
“Mkakati wa serikali kuhakikisha tatizo la ajali linapungua ni kurekebisha sheria hii ili kupunguza tatizo hili, na tupo hatua za mwisho kabisa tayari kuleta muswada wa sheria bungeni kwa ajili ya kufanyiwa kazi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba, alihoji kauli ya serikali kuhusu kuwapo na fujo ya matumizi ya barabara kwa bodaboda kutokana na watu wengi kupata ajali na hivi karibuni kuwapo kwa mbunge aliyekuwa amepanda bodaboda na kupata ajali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Sillo alitoa wito kwa watumiaji wa barabara kuzingatia sheria ya usalama barabarani ili kujiepusha na ajali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED