TRA yaunga mkono kampuni iliyolipa kodi bil 5/- miezi mitano

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 03:26 PM Dec 19 2024
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda (kulia) akimkabidhi  Tuzo ya Heshima Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited, David Mulokozi (kushoto), baada ya kuItembelea kampuni hiyo.
Picha: Jaliwason Jasson
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda (kulia) akimkabidhi Tuzo ya Heshima Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited, David Mulokozi (kushoto), baada ya kuItembelea kampuni hiyo.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kuona kodi ya Sh. bilioni tano iliyolipwa na kampuni ya Mati Super Brands Limited, kwa kipindi cha miezi mitano, imeitunuku kampuni hiyo Tuzo ya Heshima, ili kutambua mchango wake.

 Tuzo hiyo imetolewa Desemba 18 mwaka huu na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alipotembelea kiwanda cha kuzalisha vinywaji changamshi na kuongea na menejimenti ya kiwanda hicho.

Mwenda alisema kampuni hiyo ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa wa kitaifa, hivyo TRA imeona itambue mchango wake, ili kampuni iendelee na ifikie malengo yake.

Kamishna huyo alisema TRA itaendelea kuwapa ushirikiano, ili waweze kukua na kuendelea kulinufaisha taifa.

"Sisi kama TRA tutahakikisha tunaipa ushirikiano wa kutosha kampuni hii na kama kuna changamoto kusaidia kuzitatua, ili ikue na kustawi kibiashara," alisema Mwenda.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, David Mulokozi, aliipongeza TRA kwa kuwapatia ushirikiano na wanaweza kukua kwa kasi na kuweza kusambaza bidhaa zao mpaka nje ya nchi.

Mulokozi alisema kwa sasa wameanza kusafirisha bidhaa zao kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi na Zambia na ameahidi kuendelea kuzalisha bidhaa zenye kukidhi ubora.