WATALII kutoka Ufaransa na maeneo mengine ya Bara la Ulaya wanatarajiwa kumiminika kwa wingi katika Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha baada ya kuzinduliwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka jiji la Paris mpaka Kilimanjaro kupitia Zanzibar.
Kampuni ya ndege ya Air France imezindua safari hiyo mpya kuwasaidia watalii wanaopenda kufika maeneo ya kitalii hususani kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza mkoani Kilimanjaro, Meneja wa kampuni hiyo hapa nchini, Rajat Kumar, amesema safari hizo zitatoa fursa kwa muingiliano wa watu kutoka Ulaya na maeneo mingine kuibgia kwenye mikoa yenye utajiri wa utalii ya Kilimanjaro na Arusha.
"Tunayo furaha kuwapa abiria uunganisho jipya na kivutio chenye mvuto mkubwa kwa wasafiri wa matukio, wapenda asili, na watafutaji wa tamaduni," amesema Rajat.
"Njia hii mpya ni sehemu ya dhamira yetu endelevu ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya safari za Afrika na kufungua fursa zaidi za usafiri kwa watu wa ukanda huu kwenda Ulaya na zaidi, lakini pia kukuza utalii wa pande zote mbili," amesema Kumar
Amesema safari hizo mpya zitawezesha kufikia Mlima Kilimanjaro, kilele kirefu zaidi barani Afrika na eneo lililotangazwa kuwa Urithi wa Dunia na UNESCO.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED