Mahakama Kenya yabariki Jeshi kuingia mtaani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:32 PM Jun 28 2024
Bunge liliidhinisha jeshi kuwasaidia polisi katika kutuliza ghasia za maandamano.
Picha: Brian Inganga/AP/dpa
Bunge liliidhinisha jeshi kuwasaidia polisi katika kutuliza ghasia za maandamano.

MAHAKAMA nchini Kenya imeidhinisha uamuzi wa kulipeleka jeshi mitaani kuwasaidia polisi, wakati maandamano yakiendelea dhidi ya mswada tata wa kodi ambao serikali imeahidi kuuondoa.

Wakati magari ya kivita ya kijeshi yalionekana Alhamisi mjini Nairobi, mahakama imetoa uamuzi kuwa hatua ya kutumiwa jeshi iliyoidhinishwa na bunge, ni ya halali kutokana na kuzuia kwa machafuko wakati wa maandamano, ambayo polisi wameshindwa kuyadhibiti. Mahakama ilipinga rufaa iliyowasilishwa na chama cha wanasheria.

Jumanne wiki hii, waandamanaji walivamia bunge na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo. Hata hivyo Jaji Lawrence Mugambi pia alionya kuhusu kile alichosema mwenendo hatari ambao huenda ukasababisha nchi kuwa chini ya udhibiti wa jeshi. Kwa hiyo ametaka taarifa sahihi kutoka kwa serikali katika siku mbili kuhusu upeo na muda wa operesheni hiyo.

Alhamisi kulishuhudiwa maandamano katika maeneo tofauti ya nchi ukiwemo mji mkuu Nairobi. Kulikuwa na ulinzi mkali hasa katika eneo la Ikulu baada ya waandamanaji kusema walipanga kuandamana hadi Ikulu ya Rais.