WATU 27 wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kwa tuhuma za kufanya vurugu na kufunga barabara eneo la Magubike wilayani humo.
Inadaiwa wananchi hao walifunga barabara kuu ya Morogoro-Dodoma katika eneo hilo juzi, wakishinikiza serikali kuweka matuta kwenye eneo hilo baada ya kijana aliyefahamika kwa jina la Piason Senyagwa (20) kugongwa na gari na kupoteza maisha papohapo.
Akizungumza wakati wa mazishi ya kijana huyo aliyegongwa na gari na kupoteza maisha, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka alisema kuwa kutokana na vurugu hizo, mali mbalimbali zimeharibiwa na askari wawili kujeruhiwa.
Shaka aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi. Alisema kuwa tayari serikali inafanyia kazi changamoto hiyo.
Mkuu wa Wilaya huyo alisema kuwa miongoni mwa waliokamatwa, yumo dereva aliyehusika na ajali pamoja na gari lililosababisha ajali. Wanaendelea na taratibu zaidi za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Awali, Diwani wa Magubike, Abuu Msofe alisema kuwa siku ya tukio kijana huyo alikuwa anavuka barabara na kugongwa na gari.
Diwani huyo alisema kuwa kutokana na matukio hayo kujirudia mara kwa mara katika eneo hilo, wananchi wakajichukulia sheria mkononi kwa kufunga barabara kushinikiza serikali itatue changamoto hiyo kwa kuweka matuta.
Alisema kuwa baada ya kufunga barabara, askari polisi walifika katika eneo hilo na wananchi kuwarushia mawe na kufanya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi.
"Kwa kipindi cha miaka miwili, watu tisa wamegongwa na magari katika eneo hili. Tunaomba serikali isikie kilio hiki na namna nzuri zaidi ya kusadia changamoto hii ambayo imedumu kwa kipindi kirefu," alisema diwani huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED