Tabora United: Asanteni wageni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:37 PM Jan 03 2025
 Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Christina Mwagala.
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Christina Mwagala.

KLABU ya Tabora United inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imesema mafanikio waliyopata msimu huu yanatokana na 'mchango mkubwa' wa wachezaji wa kigeni waliowasajili tofauti na timu nyingine nyota wao wa kulipwa wanakosa namba katika kikosi cha kwanza, imeelezwa.

Tabora United imesajili wachezaji wageni 12, na wakati mwingine nyota hao wote wanapata nafasi ya kucheza na kuisaidia timu kufikia malengo.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa  mzunguko wa kwanza, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Christina Mwagala, amesifia usajili wao 'umelipa' na pia amewapongeza wachezaji hao wa kigeni kuzoea haraka mazingira ya soka la Tanzania.

"Nadhani sisi Tabora United ndiyo tuna wachezaji 12 ya kigeni ambao wanacheza wote, yaani kuna mechi wanaweza kucheza wote 12, waanza baadhi halafu kipindi cha pili wanaingia wengine, Hii ni kwa sababu hatukukurupuka katika usajili, timu nyingine mechi inaisha wachezaji watano au saba tu wageni ndio wamecheza, kwa sababu wengine viwango vyao ni vya kawaida sana na wanazidiwa na wachezaji wa hapa Bongo," Mwagala alisema.

Hata hivyo Mwagala alisema haina maana wachezaji wao wazawa hawana ubora, ila wote wanachuana kwa ajili ya kushawishi mwalimu kuwapa nafasi.

"Ndiyo maana utaona wachezaji wa kigeni wa Tabora United wote wanacheza na Watanzania kama, Offen Chikola pia wanacheza kwa kiwango cha juu, kwa sababu huwa tunasajili kwa kuangalia viwango na si utaifa," aliongeza ofisa huyo.