130 waliokimbia ukeketaji wagoma kurejea nyumbani

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 09:43 AM Jan 04 2025
Vifaa vya ukeketaji.
Picha:Mtandao
Vifaa vya ukeketaji.

WASICHANA 130 waliokimbia familia zao kuepukana na kukeketwa wamegoma kurejea nyumbani wakiogopa kutendewa unyanyasaji na wazazi, ndugu au walezi wao.

Wasichana hao ni waliohifadhiwa katika kituo cha ATFGM Massanga wilayani Tarime, mkoani Mara kwa lengo la kulindwa dhidi ya vitendo vya ukeketaji walivyolazimishwa kufanyiwa na wazazi wao.

Meneja miradi wa kituo hicho, Valerian Mgani alisema juzi wakati akipokea misaada iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya watoto hao, kuwa wasichana hao wameogopa kurudi nyumbani wakihofia wazazi wao kuwalazimisha kukeketwa na kuingia katika ndoa za mapema kinyume na matarajio yao.

"Wasichana hao walikimbilia hapa baada ya kulazimishwa kukeketwa na baadhi ya walezi na wazazi wao wasio waaminifu na baada ya muhula wa tohara kukamilika wamegoma kurudi kwao wakihofia kufanyiwa ukatili wa kijinsia," alisema.

Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Rais, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, aliagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Tarime kushiriki mpango wa kuwahudumia wasichana hao wakati serikali ikichukua hatua zaidi kuwanusuru.

Alisema serikali itachukua hatua kwa wazazi wote ambao watakiuka wajibu wao wa kuhudumia familia zao kwa kuzuia watoto hasa wa kike kupata elimu kwa ajili ya kuolewa kwa tamaa ya mali.

Aidha, alisema lazima jamii katika eneo hilo iachane na mila zinazoshusha hadhi ya wanawake na wasichana wadogo.

Kadhalika, aliliagiza Jeshi la Polisi kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaoendeleza ukeketaji nyakati za usiku na kuwavisha wasichana mavazi ya wanaume ili kukwepa mkono wa sheria.

Alitahadharisha baada ya shule kufunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu, kuwa serikali kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji wataanzisha msako kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanajiunga kidato cha kwanza.