Trafiki wasimamisha na kukagua gari la waziri

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 09:31 AM Jan 05 2025
Trafiki kwenye majukumu yake ya kazi
Picha: Mtandao
Trafiki kwenye majukumu yake ya kazi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesimamishwa na askari wa usalama barabarani na kukaguliwa gari alilokuwa akisafiria lenye namba binafsi katika eneo la Magugu, wilayani Babati, mkoa wa Manyara katika barabara kuu ya Babati-Arusha.

Bashungwa alisimamishwa na askari hao jana eneo la Magugu alipokuwa safarini.

Aliwapongeza askari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akisema wawaambie watu  barabarani si sehemu ya machinjio ya watu.

Alisema askari hao wanasimamia majukumu yao kwa weledi, hivyo hana budi kuwapongeza.

"Mtu yeyote anayetumia chombo cha moto ni lazima afuate taratibu na sheria za usalama barabarani," alisema Bashungwa.

Waziri huyo alisema alikuwa amekaa  nyuma anaangalia wanavyotimiza majukumu yao, walipomaliza akaona awasalimie kabla ya kuendelea na safari.

Desemba 31 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia taifa, alisema ajali za barabarani mwaka jana ziliua zaidi ya watu 1,000 na kusisitiza madereva kufuata sheria za usalama barabarani.

Ikumbukwe kuwa kikosi cha usalama barabarani kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kimekuwa kinafanya ukaguzi wa magari na kimewafungia leseni baadhi ya madereva ambao walikiuka taratibu na sheria za barabarani.