WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na serikali ikiwamo ya elimu kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Alitoa wito huo jana wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Makoba iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
Ufunguzi wa skuli hiyo ni sehemu ya shamrashamra kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema serikali imeendelea kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa elimu ikiwamo ujenzi wa miundombinu.
Aidha, alisema katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuipa hadhi sekta ya elimu kwa kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu.
“Sina shaka leo hii chini ya Jemedari Dk. Hussein Ali Mwinyi sote tunashuhudia mwendelezo wa hatua kubwa ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini. Suala hili ni la kujivunia kwa kuwa ni matunda ya Mapinduzi ambayo sasa yanafikisha miaka 61 tangu kuasisiwa kwake”.
Kadhalika, alisema serikali inayoongozwa na Mwinyi, imeendelea kufanya mageuzi makubwa ya elimu katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu nchini. “Mageuzi hayo ni pamoja na kutekeleza mtaala mpya wa umahiri utakaomwezesha mtoto kujifunza kwa vitendo na kumudu kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia”.
Alisema serikali imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na kufanya jitihada za makusudi za kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwenye sekta zote za kijamii ili kuleta tija inayotarajiwa kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi ameendeleza ari ya Waasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha analeta mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu.
“Serikali hii iliahidi kuboresha miundombinu ya madarasa kwa shule za msingi kwa kujenga madarasa 1,000 na 500 kwa ngazi ya sekondari na mpaka sasa kwa ngazi ya msingi imejenga madarasa 2,893 na ngazi ya sekondari imejenga madarasa 1,917.”
Ujenzi wa shule hiyo ambao umefikia asilimia 100 umegharimu Sh. bilioni 6.1 ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED