Vivutio vya utalii nchini kutangazwa kwenye miji 411

By Restuta James , Nipashe
Published at 02:18 PM Jan 08 2025
Vivutio vya utalii nchini kutangazwa kwenye miji 411
Picha:Mpigapicha Wetu
Vivutio vya utalii nchini kutangazwa kwenye miji 411

BODI ya Utalii Tanzania (TTB), imeingia makubaliano ya miaka mitatu kutangaza utalii kwenye ndege 490 na miji 350, nje ya Afrika.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Dar es Salaam kati ya TTB na Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Januari 07, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, amesema vivutio hivyo vitatangazwa kwenye ndege za shirika hilo zaidi ya ndege 490, ambazo zinaenda miji 411, ikiwamo 61 ya Afrika.

Amesema bodi hiyo imeingia makubaliano ya miaka mitatu na shirika hilo, ambayo pia yatatoa fursa ya kutangazwa kwa vivutio vya Tanzania kwenye tovuti zote za shirika hilo la ndege.

Amesema maeneo mengine ambayo vivutio vya Tanzania vitatangazwa ni ofisi zote za shirika hilo ambalo pia litatoa bei ya punguzo la nauli kwa watu watakaosafiri kwa ajili ya kutalii.

"Matarajio yetu ni kuongeza idadi ya watalii kuja kutembelea vivutio vingi tulivyonavyo, lakini pia kuvutia wawekezaji kwenye sekta za utalii nchini," amesema Mafuru.

Mafuru amesema mikakati yao ni kuendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ya ndege, ili kujitangaza na kuvuta watalii na wawekezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Turkish Airlines, Kadiri Karaman, ameipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na kwamba limekuwapo nchini kwa miaka 15 sasa.

Amesema shirika hilo linaitambua TTB kama mshirika mkuu wa kutangaza utalii wa Tanzania; na kwamba ushirikiano huo utasaidia kuimarisha lengo la pamoja la kuifungua Tanzania kwenye masoko ya utalii ya kimataifa kwa manufaa ya pande zote.

"Kauli mbiu yetu ndani ya shirika ni ‘Panua Ulimwengu Wako’ Tunajivunia kushikilia Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa ndege zetu kwenda nchi nyingi zaidi, hatua ambayo inasisitiza uwezo wetu wa kuunganisha watalii kutoka kila kona ya dunia hadi Tanzania," amesema.

Amesema kuanzia Juni, wataongeza safari za ndege kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kutoka nne hadi 14 kwa wiki na Zanzibar kutoka safari tisa hadi 14 kwa wiki.