UNAPOZUNGUMZIA usimamizi shirikishi wa misitu, siyo wananchi wote katika wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, sasa wanaelewa faida ya usimamizi wa misitu, ikiwa ni zao la ‘darasa misitu.’
Dhana usimamizi shirikishi wa misitu, ni mkakati wa kisera ulioanzishwa nchini, kuwahimiza wananchi katika mikoa mbalimbali, kusimamia na kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwenye ardhi za vijiji vyao.
Katika maeneo mengi nchini, mkakati huo umesaidia wananchi wengi wenye misitu ya hifadhi ya vijiji kujenga shule, zahanati, visima vya maji, wananchi kupata bima za afya, kujenga barabara, madarasa na miradi mingine kupitia usimamizi shirikishi wa misitu.
Ili wananchi waweze kunufaika na usimamizi shirikishi wa misitu kwenye ardhi za vijiji, Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa Kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wameanzisha mradi wa kuleta suluhisho la Ujumuishaji wa Misitu na Nishati Endelevu ya Tungamotaka Tanzania (IFBEST), katika wilaya ya Handeni.
Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira, kwa kuboresha usimamizi endelevu wa misitu na uzalishaji endelevu wa nishati ya tungamotaka.
MWENYEKITI MALIASILI
Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili wa Kijiji cha Gendagenda, Ali Mikumi anasema, hadi sasa kupitia mradi wa IFBEST, wananchi wamefundishwa jinsi ya kusimamia na kuhifadhi msitu.
Anafafanua katika hilo, wanatenga hifadhi ya kijiji kwa ajili ya usimamizi shirikishi wa misitu, uzalishaji mkaa endelevu, matumizi ya GPS (mfumo wa utambuzi wa maeneo duniani unaotumia satelaiti) na jinsi ya kuanzisha vikundi vya mpango hisa.
“Kutokana na elimu tuliyoipata, tumefanikiwa kutenga msitu wa hifadhi ya kijiji wenye ukubwa wa hekta 4799.5 kwa ajili ya usimamizi shirikishi wa misitu na uzalishaji mkaa endelevu, kujua umuhimu wa kuhifadhi misitu na faida zake, kuanzisha vikundi vya mpango hisa na uzalishaji mkaa endelevu,” anasema.
Anasema, ingawa wamepata elimu hiyo, kamati ya maliasili bado inahitaji kupata mafunzo ya kijeshi, ili kusimamia msitu vizuri, kupambana na wavamizi wanaoingia ndani ya msitu wa hifadhi ya kijiji kinyume na sheria kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na uchomaji mkaa.
Pia, anataja kuna changamoto ya mipaka, hakuna ‘beacon’ (mawe yaliyopandwa ardhini kuonyesha mipaka ya eneo lililopimwa) hasa mpakani mwa msitu wa hifadhi ya kijiji, bado watu wanaingia ndani ya msitu wanachoma mkaa na mbao.
“Tunaomba Halmashauri ya Wilaya ya Handeni itusaidie kuweka ‘beacon’ kwenye mipaka ya kijiji,” anasema.
Anasema, wanaomba kuwekewa ‘beacon’, kwa sababu wanakijiji watokao Mtango, Kwakibuyu na Mseko bado wanaendelea kuingia kwenye msitu kukata miti kwa ajili ya uchomaji mkaa.
Pia, wanaomba vifaa kwa ajili ya kufanya doria msituni, katika hifadhi ya kijijini Gendagenda, zikiwamo sare za Wajumbe wa Kamati ya Maliasili, buti za kutembelea porini, pikipiki na ‘GPS’.
MNUFAIKA MRADI
Zaituni Omary, ni miongoni mwa wanawake katika kijiji cha Gendagenda, Handeni walionufaika na mradi wa IFBEST.
“Tunashukuru TFCG na MJUMITA kuleta mradi wa IFBEST katika kijiji chetu, kinamama tunafanya kazi bila ya woga, tunajiamini, mradi huu umetuthamini, tunafanya kazi kwa pamoja kwenda kufanya ‘patrol’ (doria) msituni kwa kushirikiana na wanaume, tofauti na miaka ya nyuma,” anasema.
OFISA MTENDAJI GENDAGENDA
Musa Kihumbi, ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gendagenda, anasema mradi huo wa IFBEST, umesaidia kuondoa changamoto za wakulima na wafugaji katika kijiji hicho, baada ya kufahamu mipaka kati ya vijiji iliko.
“Labla ya mradi hali ya msitu ilikuwa mbaya, lakini tangu mradi uanze, msitu wetu umekuwa mzuri na sasa hivi tutaanza kufanya biashara ya hewa ukaa, uchomaji mkaa endelevu na pia hivi sasa tunatunza mazingira na msitu wetu ili tunufaike na hewa ukaa kwa kuuza ‘carbon’ (ukaa),” anasema.
Anaeleza kushukuru ufadhili wa kimataifa, kupitia Wizara ya Fedha, umewezesha kuwapo mradi huo kijijini, ikifanikishwa kupitia mpango wa matumizi ardhi.
“Hapo mwanzo katika kijiji chetu hapakuwa na msitu wa hifadhi, watu walikuwa wanaingia kwenye msitu wanakata miti ovyo, kuchoma mkaa, mbao na mifugo, lakini baada ya kuja radi tumeweza kutenga msitu wa hifadhi ya kijiji ambao tunauhifadhi kisheria,” anasema.
WENYEVITI MIRADI
Bakari Athuman, ni Mwenyekiti wa Mtandao wa MJUMIKWEKIGE, unaounganisha vijiji vitatu; Gendagenda, Kwedihawala na Kitumbi, anawashukuru wakuu wa wilaya za Pangani na Handeni na Mpima Ardhi Mkoa, kwa kuwasaidia kutatua mgogoro kati ya kijiji cha Gendagenda na Mkalamo.
Anataja bado kuna eneo lingine la mgogoro wa mipaka kati ya vijiji vya Gendagenda na Mtango; Gendagenda na Kwa Kibuyu; Gendagenda na Mbulizaga; pia Gendagenda na Mseko.
WITO MUHIMU
“Tunamwomba Kamishna wa Ardhi Mkoa, Ofisa Ardhi kutoka wilaya za Pangani na Handeni, waje kumalizia zoezi la kuainisha mipaka ya vijiji, kwa sababu zoezi la kuainisha mipaka walililisimamisha, wakisema mpaka Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uishe ndiyo watarudi tena.
“Sasa uchaguzi umeisha, tunawaomba waje kumalizia zoezi hili, ili tuweze kusimamia vizuri msitu wetu wa hifadhi ya kijiji na hatimaye tuweze kunufaika na rasilimali za misitu iliyopo katika kijiji chetu kwa maendeleo ya kijiji na wananchi kwa ujumla,” anasema Bakari Athuman, Mwenyekiti wa Mtandao unaounganisha vijiji vitatu.
DIWANI KATA MGAMBO
Hamis Mwang’ona, ni Diwani Kata ya Mgambo, anasema hadi sasa wamefanikiwa kwenda wilaya ya Tanganyika katika mkoa wa Katavi kujifunza namna kuhifadhi ya misitu, kujenga shule, pia zahanati kupitia uhifadhi wa misitu.
“Kama diwani, nipo tayari kuhakikisha misitu inaendelezwa katika kata yangu, ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali za misitu,’ anasema Mwang’obna.
Augustino Gervas, Ofisa Usimamizi Shirikishi wa Misitu, anaahidi mapato yatakayopatikana kutokana na usimamizi shirikishi wa misitu katika kijiji cha Gendagenda zitatumika kufanya doria msituni, shghuli za maendeleo ya kijiji, kununua sare za kamati ya maliasili na mafunzo zaidi kwa ajili ya doria.
“Naishukuru mradi wa IFEBEST kwa sababu TFCG na MJUMITA walitoa wataalamu wawili, yaani Ofisa Ardhi kwenda kutatua migogoro wa mipaka, kati ya wilaya ya Pangani na Handeni,” anasema.
Anasema kabla ya mradi, kijiji cha Gendagenda kilikuwa na msitu, lakini ulikuwa haujatengwa kama wa hifadhi ya kijiji.
Hadi sasa wilaya ya Handeni imefanikiwa kutenga hekta 1,060 za misitu kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa endelevu, katika vijiji vya Gendagenda na Mkalamo.
OFISA MALIASILI
Napoleon Mlowe, ni Ofisa Maliasili Wilaya ya Handeni, ana maelezo yake kuwa: “Tunaishukuru MJUMITA na TFCG kuja katika wilaya yetu, mradi huu wa IFBEST unaotekelezwa katika vijiji vitatu; Kijiji cha Kwa Msisi, Gendagenda na Mkalamo na umelenga zaidi katika misitu ya vijiji.”
Anasema, kupitia mradi, wamepewa elimu kuhusu uhifadhi wa msitu na namna wanavyoweza kunufaika na msitu, mazao ya msitu na elimu ya utawala bora.
Mlowe anasema mradi umeshabadilisha jamii zote, kiuchumi, kijamii na matokeo kubwa ya wanalohitaji ni vijiji wapate mapato kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Pia, kupitia mradi huo, anaahidi wananchi wataanza kujihusisha na biashara ya hewa ukaa kupitia uhifadhi wa misitu.
Lingine, anaahidi kupambana na mabadiliko ya tabianchi, pia jamii kunufaika na mapato ya rasilimali za misitu.
“Kama Wilaya ya Handeni, tumetenga shilingi milioni 15 kusaidia shughuli za uhifadhi wa misitu ya vijiji,” anasema Mlowe.
Pia, anataja vikundi vya mpango hisa ambavyo vimeanzishwa, wilaya ya Handeni itaelekeza kiasi cha fedha kielekezwe kwenye vikundi hivyo.
Dhamira anataja ni kusaidia vikundi vinavyofanya shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwamo misitu waweze kupata mkopo wa asilimia 10.
Mapato ya ndani yataendelea kupangwa kwenye shughuli za uhifadhi wa misitu, hadi sasa wilaya ya Handeni ina vijiji 91na ina misitu ya vijiji 32,000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED