CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetoa tathmini ya mwaka 2024, kikikumbusha matukio 12 ya kupotea kwa raia, huku kikijinasibu kusimamia mambo matano mwaka huu.
Aidha, kimeita vyama vingine vya upinzani kushirikiana ili kuweka mikakati ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Isihaka Mchinjita, alisema matukio ya kupotea kwa watu, yaliwapitisha wananchi kwenye mateso makubwa.
Mchinjita alisema, matukio ya kutekwa na kuuawa kwa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Kibao, kuwa miongoni mwa matukio yaliyowaumiza wananchi.
Alitaja watu wanaodaiwa kutoweka kuanzia Januari Mosi, mwaka jana, kuwa ni William Herman, David Lema, Yonzo Shimbi, Lilenga Isaya, Simoni Nairiam, Edgar Mwakalebela, Abdul Nondo, Deusdedit Soka, Frank Mbise, Jacob Mlay na Shadrack Chaula.
“Licha ya matukio yote haya ya wazi kabisa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote ya kina kuhusu matukio haya licha ya Rais kutoa maelekezo ya kuchunguzwa,” alisema.
“Baraza Kivuli la Mawaziri ninaloliongoza litaenda kuhakikisha Watanzania wanachagua mabadiliko ya kweli, yatakayowatoa kwenye uonyonge, uonevu na dhuluma,” aliongeza.
Mchinjita alisema kwa mwaka huu, chama hicho kimeazimia kupigania mageuzi ya kidemokrasia, kupinga sheria kandamizi, kujenga taifa la wote, haki za ardhi kwa wananchi, huduma za matibabu kwa wote, hifadhi ya jamii kwa wananchi wote, haki za wafanyabiashara ndogo ndogo na bei nzuri ya mazao kwa wakulima.
Mchinjita ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, alikumbusha kuwa mwaka 2025 ni wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo kuwataka wafuasi na viongozi wa vyama vingine vya upinzani kuunganisha nguvu ili kuikabili CCM.
“ACT Wazalendo imedhamiria kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote. Si taifa la wachache wanaofaidi keki ya taifa gharama za wananchi wa kawaida, si taifa la watu wachache tu ndio wenye hakika ya matibabu, pensheni na viinua mgongo, si taifa la watu wachache ndio wenye haki ya kuishi kwa furaha. Sio taifa la viongozi ndio wanaoneemeka.
“ACT Wazalendo tunatoa wito kwa vyama makini vya upinzani, tukae pamoja na kujadiliana namna bora ya kuikabili CCM, tunahitaji umoja na mshikamano thabiti wa kuwahakikishia watanzania kuwa tuko tayari kuwapa matumaini,” alisema Mchinjita.
Kuhusu gharama kubwa ya matibabu na kupendekeza kuwa serikali ije na mpango wa bima ya afya kwa wote.
“Huduma za afya zinapaswa kuwa haki inayopatikana kwa kila mtu bila kujali hali yake ya kifedha. ACT -Wazalendo tunaitaka serikali kuwekeza fedha ili kugharamia matibabu kwa watu wote nchini kwa kuwapatia Watanzania wote bima ya afya isiyo na matabaka,” alisema.
Alisema gharama kubwa za matibabu zinaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wengi. Alipendekeza pia serikali iajiri walimu, madaktari, wauguzi na wataalamu wa kilimo, ili wananchi wapate huduma bora za kijamii za uhakika.
Kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma, Mchinjita alisema chama hicho kinaitaka serikali iwachukulie hatua wahusika na kwamba hatua hiyo itadhibiti mianya ya wizi serikalini.
Aidha, kuhusu mikopo umiza, alisema ripoti zinaonesha kuwa wanaoumia ni wananchi wenye kipato cha chini na kuitaka serikali kutengeneza sera madhubuti ili kudhibiti utoaji mikopo kiholela.
“Kukosekana kwa mifumo salama ya mikopo kunawafanya wananchi kukosa fursa za kiuchumi, huku taasisi za kifedha zikiendelea kunufaika kwa kuwanyonya wananchi,” alisema.
Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, alisema ACT-Wazalendo iliamini R4 za (Maridhiano, ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya Taifa), zingetumika kuimarisha demokrasia, lakini imekuwa kinyume chake.
Alisema kutokana na kutoridhishwa na uchaguzi huo, tayari kimefungua kesi 51 katika maeneo mbalimbali nchini, kuupinga.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, alisema chama hicho kitatumia mbinu zingine kumkabili mgombea wa CCM.
“Bila kufanya hivyo au kwa kudhani kwamba kuna maridhiano, tutaingia kwenye hadaa na kucheza mchezo mchafu ambao unaweza kuiharibu nchi yetu,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED