RAJABU Reli (22) amehukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kuvaa na kutembea na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kinyume cha sheria.
Shauri hilo la jinai namba 445/2025 lilitolewa hukumu juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Evodius Kisoka.
Awali akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 5, 2024 katika kijiji cha Kasisa, Wilaya ya Sengerema kinyume cha kifungu cha 178(1) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, SURA 16, marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani huko Januari 7, 2025 na kusomewa shtaka la kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania bila ruhusa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mshtakiwa huyo alikiri kosa na kueleza kuwa alifanya hivyo ili aweze kukubaliwa na mchumba wake na kuwa kosa hilo amelifanya mara moja tu.
Mahakama hiyo ilipokea ushahidi wa sare hizo alizokuwa akizivaa kisha kusikiliza pande zote za ushahidi ambako Hakimu Kisoka alijiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni mzito na haukuacha shaka lolote.
Hakimu Kisoka alitoa nafasi kwa mshtakiwa huyo kujitetea kwanini asipewe adhabu kali. Naye akaomba mahakama hiyo imwachie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.
"Mheshimiwa Hakimu, ninaomba nisamehewe kwa kuwa ni kosa la kwanza na nilivaa na kwenda kumwonesha mchumba wangu kuwa mimi ni askari ili asinikatae," alidai Rajabu.
Hata hivyo, Hakimu Kisoka alitupilia mbali ombi hilo na kutoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Rajabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED