Mnyika atangaza wiki mbili na masharti uchaguzi CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:38 AM Jan 08 2025
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza wiki mbili za kujifungia kwenye vikao vya kuwapata viongozi wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Januari 22 mwaka huu.

Vilevile, kimetoa tahadhari kwa wanachama, wagombea na mawakala au wapambe wao, kuzingatia Katiba, miongozo, kanuni, taratibu na itifaki ya chama hicho katika mchakato mzima wa uchaguzi na kwamba ipo hatari ya wagombea kuondolewa katika kinyang`anyiro endapo itathibitika kukiuka hayo.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ndiye alitangaza hayo jana wakati anazungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya chama hicho mkoani Dar es Salaam.

Alisema vikao hivyo ni vya usaili na uteuzi wa wagombea pamoja na uchaguzi wenyewe.

"Kwa kweli tutakuwa na vikao vya chama mfululizo, ni ‘marathon' ya vikao vya kama wiki mbili hivi, vitahusisha usaili, uteuzi wa wagombea na baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, kutafuata hatua ya uchaguzi wenyewe," alisema.

Alisisitiza kwamba kuelekea katika uchaguzi huo, wanachama, wagombea pamoja na mawakala wao, wanatakiwa kuzingatia Katiba, kanuni, miongozo, taratibu na itifaki ya chama hicho.

"Wakati ninatoa tangazo la uchaguzi, nilitoa wito kwa wagombea, wanachama na mawakala wa wagombea, kuzingatia Katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama katika mchakato mzima wa uchaguzi na mahususi nilitaka wazingatie miongozo miwili muhimu ya chama katika kipindi hiki cha uchaguzi ambayo ni ule unaohusiana na taratibu za kuendesha kampeni ya uchaguzi ndani ya chama na ya rushwa yote ya mwaka 2012.

"Hata hivyo, katika kipindi hiki cha uchukuaji na urudishaji fomu, kumejitokeza vitendo ambavyo vinaashiria kuvunjwa kwa miongozo hii na baadhi ya wanachama au wagombea, kuna tuhuma za namna mbalimbali za namna hiyo," alisema Mnyika.

Aliwataka kusoma masharti ya msingi yaliyomo katika miongozo hiyo na kwamba iwapo kuna kiongozi, mwanachama au mgombea atakayeikiuka, malalamiko yawasilishwe katika ofisi yake ili hatua zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.

"Kwa masharti yanayohusu taratibu za kampeni, CHADEMA ni chama kinachoamini katika demokrasia, usawa na maadili ya kweli na kwa kuwa maadili ya chama ndiyo yanayoainisha sifa za uongozi wa chama.

"Sifa hizo ambazo ni pamoja na nidhamu, utii, uwajibikaji na dhamira ya wanachama, viongozi na chama katika ngazi mbalimbali kwa muundo wa chama na jinsi ya kuwapata na kuwapima viongozi. 

"Hivyo basi, mwongozo huu unalenga kuhakikisha kuwa kampeni zinafanyika kwa uwazi, haki na kwa kufuata misingi ya demokrasia," alisema Mnyika.

YASIYOTAKIWA

Mnyika alisema wagombea au mawakala wao wakati wa kampeni, wanatakiwa wafuate taratibu kwa kutofanya kampeni hizo kabla ya muda wake kutangazwa na mamlaka husika ndani ya chama hicho.

Pili, mgombea au wakala wake, kama ilivyosisitizwa na Mnyika, hatoruhusiwa kufanya kampeni chafu kwa kumkashifu mgombea mwenzake kwa kusambaza nyaraka, vipeperushi au taarifa kwa njia ya mitandao ya kijamii zisizohusiana na wasifu wake.

Tatu, Mnyika alisema ni marufuku kusambaza taarifa kwa njia yoyote ile zenye lengo la kukashfu mgombea au kiongozi wa chama na sharti la nne ni marufuku kwa mgombea au wakala wake kufanya kampeni kwa kuhusisha ukanda, udini ukabila au ubaguzi wa aina yoyote ile.

"Tano, mgombea au wakala wake, anatakiwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika mwongozo dhidi ya rushwa. Sita, mgombea au wakala wake atatakiwa kuwa na sifa kama zilivyoainishwa na Katiba na kanuni za chama hicho.

"Saba, mgombea au mwakilishi wake hatoruhusiwa kufanya kampeni kwa kujinasibu na kiongozi yeyote wa kitaifa, wilaya au kiongozi yeyote wa kuchaguliwa iwe kwa mazuri au kwa mabaya," alisema.

Mnyika alitaja adhabu za ukiukaji mwongozo na kanuzi hizo kuwa ni pamoja na kupewa onyo, onyo kali kwa kosa la pili na kwa kosa la tatu ataondolewa katika mchakato wa uchaguzi endapo itadhibitika kuwa mgombea kufanya makosa hayo.

Adhabu ya nne, Mnyika alisema ni kufungiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho kwa muda utakaotajwa na mamlaka husika usiozidi miaka mitano.

KUDHIBITI RUSHWA

Mnyika, akizungumzia mwongozo wa kudhibiti rushwa katika kampeni za chama hicho, alisema mwanachama, kiongozi au wakala wake hawaruhusiwi kutoa fedha kwa njia yoyote ile, vyakula, vinywaji au zawadi nyinginezo kwa wajumbe au wapigakura kwa lengo la kujipatia kura.

Alisema mwongozo huo unakataza kuwasafirisha wajumbe au wapigakura kuhudhuria mkutano au kituo cha kupigia kura kwa ngazi husika kwa ajili ya uchaguzi kwa lengo la kujipatia kura.

Alisema mwongozo huo pia unakataza kutoa ahadi zenye lengo la kuwalipa fadhila wajumbe au wapigakura baada ya kupiga kura kukamilika, kuandaa kikao chochote cha wapigakura kwa lengo la kuwapa fedha, chakula au zawadi zingine bila kuzingatia taratibu za kampeni zilivyoainishwa na kutoa au kushinikiza, kupokea au kushawishi rushwa ya ngono.

Mnyika alisema alisema mwongozo huo pia unakataza kutumia mamlaka ya uongozi kwenye chama kupendelea upande mmoja wa mgombea na kutumia dhamana ya uongozi ili kujinufaisha binafsi kisiasa au kimali wakati wa uchaguzi.

"Mtu yeyote anayetuhumiwa kufanya kosa ndani ya CHADEMA, mwanachama au kiongozi, kabla hajachukuliwa hatua, anatakiwa kuandikiwa tuhuma zake na kupewa nafasi ya kujitetea halafu vikao vya uamuzi vifanye uamuzi kwa mujibu wa mamlaka za kinidhamu za kuchukua hatua husika," alisema Mnyika.

Katibu Mkuu huyo alisema Katiba ya chama hicho imetoa mamlaka kwa kamati ya wazee wastaafu kusimamia uchaguzi huo, akidokeza kuwa "kulikuwa na maneno kwamba labda kura zitakwenda kuhesabiwa kwa kificho na utaratibu mwingine, niwahakikishie kwamba kura zitahesabiwa kwa uwazi palepale ukumbini."

Kuhusu wajumbe wa Kamati Kuu walioonesha mapenzi au upande wao wanaounga mkono, Mnyika alisema  hiyo si shida kwa sababu uamuzi unafanywa na kamati nzima.

Jumla ya wagombea 300 wamerejesha fomu ya kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mabaraza yake.

Kwa nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, aliwataja wanaogombea kuwa ni Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Odero Charles.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, wanaogombea ni Ezekiel Wenje, John Heche na Mathayo Gekul wakati Makamu Mwenyekiti Zanzibar wagombea ni Said Mzee Said, Said Issa Mohamed, Suleiman Makame Issa na Jafidh Ally Salehe.

Mnyika alisema usaili na uteuzi kwa wagombea wote wa mabaraza ya chama hicho utafanywa na Kamati Kuu katika kikao chake kitakachofanyika Januari 10 na 11. Alisema uchaguzi wa mabaraza hayo utafanyika kuanzia Januari 13 mpaka 16.

Alisema usaili na uteuzi kwa kwa wagombea wa nafasi za uongozi katika chama, utafanyika Januari 19 na kwamba kabla ya hapo utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu.

Alisema kuwa Januari 20 kutafanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama kwa ajili ya kuandaa ajenda za Mkutano Mkuu wa chama na Januari 21 Mkutano Mkuu wa chama na Januari 22 kutakuwa na Mkutano wa Baraza Kuu la Chama.