Tarehe kumpata mrithi wa Kinana CCM yatajwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:51 AM Jan 08 2025
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM), Amos Makalla.
Picha:Ibrahim Joseph
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM), Amos Makalla.

NAFASI iliyoachwa wazi na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana inatarajiwa kuzibwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama hicho uliopangwa kufanyika Januari 18 na 19 mwaka huu jijini Dodoma.

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM), Amos Makalla alibainisha hayo jana jijini hapa alipozungumza na waandishi habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo.

"Ajenda ya kwanza kwenye Mkutano Mkuu huu wa Taifa ni kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara. Kama mnavyojua kuwa nafasi hii ipo wazi baada ya Abdulrahman Kinana kuomba kupumzika. Kwa hiyo Mkutano Mkuu huu tutautumia kujaza nafasi hiyo iliyo wazi.

"Ajenda ya pili itakuwa kupokea kazi za chama katika kipindi cha 2022 hadi 2025. Kwa hiyo mkutano mkuu utapokea kazi za chama zilizofanyika katika kipindi hiki baada ya uchaguzi ndani ya chama 2022 hadi tulipo sasa," alisema.

Makala alisema ajenda ya tatu itakuwa ni kupokea taarifa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi kwa kazi zilizofanywa na serikali zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zile zilizofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Kwa hiyo hizo ndizo ajenda tatu lakini pia nimeeleza tarehe ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu. Nitumie nafasi hii kusema kwamba kumekuwa na ubashiri mwingi kwenye vyombo vya habari, unaona vichwa vya habari kwamba CCM ni patashika, wafuatao watajwa kuritihi nafasi ya Kinana.

"Wengine nani wanasema nani kati ya hawa atarithi nafasi ya Kinana, wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema kwamba wafuatao wajitokeza kurithi nafasi ya Kinana. Kwa hiyo kila mmoja anaandika anavyotaka," alisema Makala.

Alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti haigombewi wala mtu hajazi fomu, hivyo kusema ni kinyang’anyiro si sahihi.

"Nafasi hi haigombewi wala mtu hajazi fomu kuomba kuchaguliwa, nitakushangaa kwa nafasi ambayo haigombewi na wala hujazi fomu kinyanyang’anyiro hicho kinatoka wapi," alisema.

Makala alisema mrithi wa Kinana atapatikana kutokana na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kupendekeza jina ambalo litawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu na hapo ndipo zitapigwa kura za ndiyo na hapana ili kumpata Makamu Mwenyekiti.

"Kwa hiyo wale ambao walikuwa wakibashiri na kupiga ramli sasa muda huo haupo, huo ndiyo utaratibu wa kumpata Makamu Mwenyekiti, unapendekezwa, inawezekana miongoni mwenu tuna Makamu Mwenyekiti wa Bara humuhumu mlipo," alisema.

Alisema kikao cha Kamati Kuu na kile cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa vinatarajiwa kufanyika Januari 16, 2025 ambapo ndipo litapatikana jina hilo kabla ya kupelekwa kwenye Mkutano Mkuu.

Mwenezi huyo alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na hivi sasa wanajiandaa kuwapokea wajumbe wa mkutano huo na waalikwa watajulishwa.

Ilitangazwa kuwa Kinana aliandika barua kuomba kustaafu kwenye nafasi hiyo tangu Julai mwaka jana kwa madai ya kutaka kupumzika. Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliliridhia ombi hilo.