ELIMU ya mpigakura ni mafunzo ya uelewa anaopewa mwananchi hasa aliyejiandikisha kushiriki kuchagua viongozi kwa lengo la kuwezesha kuelewa sheria, kanuni na taratibu za mchakato mzima wa uchaguzi uwe mkuu au wa ngazi inayohusika.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kubwa linalolengwa ni kujua wajibu wa raia na umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa kuwapigia kura viongozi wanaowataka na si kuharibu kura.
Vilevile kifurushi cha elimu ya mpigakura kinaambatana na taarifa inayomwelekeza afahamu ni wapi atapigia kura, atasoma wapi jina lake na kituo, muda gani, siku na kitu gani hasa anafanya akiwa na karatasi la majina ya wagombea.
Kwa sasa Watanzania wanachosubiri ni kusikia tarehe rasmi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuwapata rais, wabunge, wawakilishi na madiwani kwa Bara na Zanzibar.
Kwa CCM, mchakato wa wanachama kuchukua fomu za kuomba kupitishwa kuwania nafasi hizo umefanyika wakisubiri mchujo na wakati wowote kuanzia sasa majina ya waliopitishwa yatatangazwa na baadaye zitafuatia taratibu nyingine ili kuandaa kampeni.
Baadhi ya vyama vingine vya siasa wagombea wanaendelea na kuonyesha nia na kuandaa wajumbe kwa ajili ya mchujo wa kupendekeza wagombea nafasi hizo.
Mathalan, ACT Wazalendo, CUF, CHAUMMA na NCCR-Mageuzi na ADC. Kufanikisha uchaguzi ni jukumu la wadau wakiwamo Asasi za Kiraia (AZAKI), ili kutoa elimu ya uraia na kwa sasa zipo baadhi zimepewa jukumu la kuuelimisha umma umuhimu wa kushiriki uchaguzi na namna ya kupigakura kwa ufanisi.
Mathalani, mkoani Pwani, Kaimu Katibu Tawala, Nsajigwa George, anasema mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, hivyo AZAKI zinapaswa kufanya kazi kwa kufuata taratibu na miongozo ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Anayakumbusha hayo mjini Kibaha hivi karibuni wakati akifungua kikao kazi cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCONGo),mkoa wa Pwani.
“Katika kipindi hiki kinachoelekea kutajwa tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, mashirika ya kiraia yaepuke kufanya shughuli au kutoa taarifa zinazoleta taharuki,” anasema George. George anaongeza:”Mashirika haya ni nguzo ya maendeleo.
"Tunayategemea kusaidia wananchi wetu, lakini pia yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhimiza amani, mshikamano na utulivu.”
Anasema asasi hizo zisibadilike na kuwa sehemu ya migawanyiko ya kisiasa au kuchochea taharuki, na kwamba serikali inazitegemea katika kulinda amani na utulivu, ambayo ni tunu ya taifa ambayo kila mmoja ana wajibu wa kuilinda.
“Serikali haitasita kuchukua hatua kwa asasi ambayo itaonekana kwenda kinyume na kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi. Hivyo fanyeni kazi zenu kwa kuzingatia hatua zote zinazotakiwa,” anasema.
Kaimu katibu tawala anayefafanua kuwa AZAKI ni wadau muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo, kuimarisha ustawi wa jamii, na kutekeleza malengo ya dira ya maendeleo ya taifa pamoja na mikakati ya kupunguza umaskini.
Kuhusu hali ya utendaji kazi wa asasi hizo mkoani humo, anasema Pwani ina mashirika ya kiraia 364, lakini yanayofanya kazi ni 108 ambayo ni sawa na asilimia 29.6, huku mengi taarifa zake hazijulikani.
Serikali mkoani humo inafuatilia kujua ni kwa nini asasi nyingi hazifanyi kazi ili kuchukua hatua kulingana na sababu zinazotajwa kuchangia zishindwe kutimiza wajibu, anasema.
Anahoji yalipo mengine na yanafanya nini, akieleza kuwa wanafuatilia kujua kuna nini ili wachukue hatua kulingana na ushahidi. Mjumbe wa Baraza Kuu la NaCoNGo, mkoa wa Pwani , Prisca Ngweshemi, anatoa kilio cha mashirika hayo na kutaka yasaidiwe.
Anasema ingawa ni wadau muhimu katika maendeleo kwenye maeneo yao, lakini wanabaguliwa kwenye vikao vya halmashauri kitendo ambacho kinawakatisha tamaaa.
“Hayo ni madai ya baadhi ya viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wanasema hawashirikishwi katika vikao vikiwamo vya mabaraza ya ushauri,” anadokeza Prisca.
Mjumbe huyo anaeleza kuwa mashirika hayo yanafanya kazi na serikali kwa karibu, huku akiongeza kuwa ushirikiano huo ni wa muhimu, kwa kuwa wote ni wadau wa maendeleo ya Watanzania.
“Lakini pia kuna usumbufu mwingine kwenye halmashauri, kwani viongozi wa mashirika wanapopeleka barua za kuomba kufanya mradi, wanapigwa danadana nyingi kupata vibali hivyo,” anasema mjumbe wa NaCoNGO.
Katika hilo, George anatoa maagizo kwa viongozi wa halmashauri kutosumbua asasi hizo na pia kuzisihirikisha kwenye vikao kwa kuwa ni wadau wakubwa wa kimaendeleo kuanzia ngazi za vijiji.
"Lakini pia suala la vibali vya kufanya kazi kuzuiliwa na wataalam wa halmashauri, wasilisheni makalamiko katoka ofisi yangu ili tuyafuatilie kwa lengo la kujua chanzo cha tatizo,” anasema.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini Mkuu kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Charles Komba, anasema ipo haja kwa viongozi wa asasi za kiraia na wa halmashauri kuaminiana na kushirikiana.
Komba anasema anashangaa kusikia kuwa mtu anafika kwenye halmashauri kuomba kibali cha kufanya kazi katika jamii ananyimwa au hashirikishwi kwenye vikao ambavyo wanatakiwa kuwamo.
“Jambo la msingi ni kujenga mahusiano mema. Kuweni na ukaribu na viongozi hao na mfahamiane vizuri, kila mmoja asiwe na mashaka na mwenzake,” anasema Komba.
Aidha, Komba anasema asasi hizo pia zinatakiwa kutoa taarifa sahihi za kifedha na idadi ya walengwa waliowafikiwa kwenye ngazi ya mkoa, ili kujijenga uaminifu kwa wahisani.
“Serikali inatambua umuhimu wa mashirika yasiyo ya kiserikali ndiyo maana imeandaa miongozo mbalimbali ikiwamo Mwongozo wa Mchango wa AZAKI na ushirikishwaji wao katika vikao vya ngazi ya kata, wilaya na mkoa na kuandaa mfumo wa usajili wa kielektroniki wenye ufanisi zaidi,” anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED