Wanasayansi wanavyoendelea kukuna vichwa vita na malaria

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:44 PM Jul 15 2025
Mbu. Wanasayansi watengeneza ukungu wa kijenetiki unaoteketeza 99% ya mbu wanaoeneza malaria
Picha; Mtandao
Mbu. Wanasayansi watengeneza ukungu wa kijenetiki unaoteketeza 99% ya mbu wanaoeneza malaria

UTAFITI mpya unaofanywa na wanasayansi wa Tanzania na Ireland unathibitisha kuwa mbu jamii ya Anopheles arabiensis, wanaoeneza malaria, huvutiwa zaidi na binadamu.

Ni tofauti na Anopheles quadriannulatus, ambaye hana mvuto huo hata kidogo, yanasema matokeo ya utafiti huo, yaliyochapishwa hivi karibuni katika jarida la Royal Entomological Society. 

Utafiti huo unaonyesha kuwa tabia ya mbu kuvutiwa na binadamu ndiyo msingi wa uwezo wao kusambaza malaria, hivyo, kuelewa aina ya mbu na upendeleo wao kwa watu ni hatua muhimu katika kuboresha mikakati ya udhibiti wa ugonjwa huo.

Utafiti huo umeendeshwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Ifakara (IHI) na Chuo Kikuu cha Cork cha Ireland, ukiongozwa na mwanasayansi Deogratius Kavishe. Ukisimamiwa na Profesa Gerry Killeen, na kushirikisha wanasayansi wengine wakiwemo Katrina Walsh, Rogath Msoffe, Lily Duggan, Lucia Tarimo, Fidelma Butler, Nicodem Govella na Emmanuel Kaindoa. 

Utafiti huo ukiendeshwa kwenye mazingira mbalimbali kuanzia maeneo ya kilimo yenye watu wengi hadi sehemu za hifadhi zisizokuwa na shughuli nyingi za kibinadamu. 

Wanabaini kwamba ingawa mabuu (funza) wa aina zote mbili wa mbu hupatikana kwa wingi kwenye maji, ni Anopheles arabiensis pekee aliyenaswa kwa wingi akiwa mbu mzima karibu na watu. 

Kwa upande mwingine, Anopheles quadriannulatus hakuonekana kuvutiwa na kuwepo kwa binadamu, unasema utafiti na kuongeza “Anopheles arabiensis anaonesha mvuto mkubwa kwa binadamu na anapatikana zaidi kwenye mitego  iliyopo  karibu na watu, hata kama mabuu ya quadriannulatus ni mengi kwenye mazingira hayo hayo,” anasema Kavishe, mwandishi mkuu wa utafiti. 

Hata hivyo, wanasayansi hao wanabaini kwamba uwepo wa binadamu umeathiri kwa kiasi fulani matokeo ya mitego na hii ni baada ya watafiti kupiga kambi porini na kuweka mitego ya mbu karibu na mahema ya watu na maeneo yasiyo na watu. Matokeo yakaonesha kwamba kwa mitego iliyo karibu na binadamu, ilinasa mbu jamii ya arabiensis mara 20 zaidi ya quadriannulatus. 

Kwa mitego iliyokuwa mbali, ambayo ilitembelewa mara kwa mara na watafiti ilionesha kuvutia  arabiensis zaidi, jambo linaloonyesha kuwa hata uwepo wa binadamu wa muda mfupi una athari. 

Wanatahadharisha kuwa uwepo wa binadamu (hata watafiti), unaweza kuathiri matokeo ya ufuatiliaji wa mbu na kupotosha takwimu. 

Kwa upande mwingine, quadriannulatus, ambaye haenezi malaria, anapatikana zaidi kwenye mitego iliyowekwa maeneo ya asili yenye utulivu bila binadamu. 

Wanasayansi hao wanaona kwamba matokeo hayo yanatoa mwanga katika vita dhidi ya malaria, kwa kuwa yanasaidia kuelewa tabia ya mbu wanaosambaza ugonjwa huo na hivyo kuwezesha kubuni mikakati madhubuti ya kuudhibiti. 

“Mikakati ya kudhibiti malaria inapaswa kuzingatia tabia za aina mahususi za mbu, ikiwemo upendeleo wao kwa wenyeji na ushindani baina yao. Hii itaongeza ufanisi wa programu za afya ya umma.” 

Utafiti unaongeza. Wanayansi wanapendekeza kubuni mbinu bora zaidi za kudhibiti mbu kwa kulenga kwa usahihi maeneo na aina ya mbu  hatari zaidi kwa binadamu. 

Katika kubaini tofauti hizo za mbu, wanasayansi hao wanatumia muundo wa utafiti wa ‘rolling cross-sectional’ kwa awamu nne za uchunguzi, zilizofanyika kwa kipindi cha miaka miwili. Ili kuleta ufanisi na tija, wanaweka kambi 40 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Eneo la Usimamizi wa Wanyamapori la Ifakara-Lupiro-Mang’ula pamoja na vijiji vya jirani. 

Jumla ya mbu wakubwa 22,525 wanakusanywa kwa kutumia mitego ya kuwanasa, ambapo aina ya mbu pamoja na asilimia zake kwenye mabano ni 5,366 (23.8), wanatambulika kimwonekano kama kundi la An. gambiae, 333 (1.5) wanaopatikana ni Anopheles funestus, 2,995 (13.3), aina nyingine za Anopheles na 13,822 (61.4) aina mbalimbali za mbu wa culicine. 

Matokeo hayo yanaonesha kuwa idadi kubwa ya mbu jike An. Gambiae, waliokamatwa (takriban asilimia 96), walikuwa hawajashiba damu, ikionyesha kuwa njia zilizotumika kuwakamata, zilifanikiwa kuwanasa zaidi mbu waliokuwa wanatafuta mtu wa kunyonya damu.

Wanasayansi hao wanaangazia tofauti za kitabia kati ya An. arabiensis na An. Quadriannulatus; ambapo An. arabiensis huonyesha mvuto mkubwa kwa binadamu,  wakati An. quadriannulatus, ambaye ndiye aliyetawala katika idadi ya kwenye mifumo ikolojia ya asili isiyosumbuliwa, haonyesha mwitikio huo. 

“Kushindwa kuwakamata mbu wakubwa wa An. quadriannulatus, licha ya wao kutawala kwa idadi kwenye maeneo ya utafiti, kunaonyesha changamoto ya kimkakati katika ufuatiliaji na udhibiti wa maambukizi ya malaria yanayobaki pamoja na wale mbu wanaoweza kuhamisha magonjwa ya wanyama kwa binadamu. 

Matokeo yanaonyesha kuwa An. arabiensis wanaswa kwa wingi karibu na binadamu, hasa katika mitego ya mwanga iliyowekwa karibu na mahema ya watafiti, hali iliyoashiria kuwa An. Arabiensis, huvutiwa zaidi na harufu ya watu. Vilevile, mtego wa wavu unaowekwa mbali na kambi walizokaa watafiti, lakini ukitembelewa mara kwa mara na watafiti ili kukusanya mbu wazima walionaswa, uliweza pia kunasa idadi kuwa ya An. arabiensis. 

Kwa upande mwingine, An. quadriannulatus walinaswa kwa idadi ndogo, hata katika maeneo ambayo viluwiluwi vyake vilipatikana kwa idadi kubwa. 

“Kwa ujumla, matokeo yanaonesha kuwa mitego ya mbu iliyokaribu na watu huvutia zaidi mbu wanaopendelea damu ya binadamu. Pia inawezekana kwamba  watafiti walipokuwa wakitembelea mtego wa wavu, ili kukusanya mbu, walisaidia kwa bahati mbaya kuwavutia mbu wa aina hiyo. 

Hii ni muhimu kuelewa, ili kuboresha njia za kukusanya mbu kwa usahihi na kupanga mikakati bora ya kudhibiti malaria. Watafiti wanatoa majibu hayo, wakati utafiti mwingine uliofanyika visiwani Zanzibar, ukipendekeza kuwa kuangamiza mbu katika mazalia yake kwa kutumia viuatilifu vya kuua viluwiluwi katika hatua za awali. 

Takwimu za serikali za mwaka jana zinaonesha kwamba kiwango cha maambukizi ya malaria nchini kimepungua na kufikia asilimia 8.1 kwa mwaka 2023, kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2015. Ili kufikia asilimia sifuri ya maambukizi, serikali mkakati wa kutokomeza mazalia ya mbu na kuhakikisha upatikanaji wa vitendanishi na dawa za kutibu malaria katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini. 

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Songwe, Manyara, Kilimanjaro, Singida na Mwanza; inatajwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo hadi asilimia moja. 

Aidha, mikoa ya Katavi, Tabora na Kagera bado ina changamoto ya kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria kutokana na hali ya kimazingira ya mikoa hiyo.