Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imewafunda maofisa uchaguzi 119 wa ngazi ya majimbo kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, namna ya kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.
Dk. Zakia Abubakar, Mjumbe wa INEC, akizungumza leo (Julai 15,2025) wakati akifungua mafunzo kwa Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa Ununuzi, Kituo cha Moshi Mjini, amesema:
“Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,”amesema Dk. Zakia.
Mjumbe huyo wa INEC, amewakumbusha kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema, ili kubaini mahitaji maalumu ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Stanslaus Mwita, amewataka watendaji hao kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria, kanuni, na maelekezo mbalimbali ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa muda wa siku tatu kwenye mikoa mbalimbali nchini, na yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.
INEC, imeyagawa mafunzo hayo katika awamu mbili ambapo awamu hii ya kwanza inahusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED