Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia chama hicho. Nondo amekabidhiwa fomu hiyo leo, Julai 15, 2025, na Katibu wa Jimbo la Kigoma Mjini, Iddi Sumvya.
Leo ikiwa ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu kwa mujibu wa ratiba ya chama katika jimbo hilo, Nondo anakuwa mwanachama wa pili kuchukua fomu ya kuwania ubunge, akiungana katika kinyang’anyiro na kiongozi wa chama huyo mstaafu, Zitto Kabwe.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Nondo amesema kuwa amezingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 21 pamoja na Katiba ya ACT-Wazalendo Ibara ya 11(c), toleo la mwaka 2024.
“Ndugu wananchi na wanachama wa ACT Wazalendo Kigoma Mjini, kama mnavyofahamu, siyo mara yangu ya kwanza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ndani ya chama kugombea Ubunge. Julai 5, 2020, nilichukua fomu katika hatua ya kura ya maoni, lakini kura zangu hazikutosha, na hivyo kiongozi wa chama mstaafu, Mh. Zitto Zuberi Kabwe, alipita kuwa mgombea wetu,” amesema Nondo.
Ameongeza kuwa dhamira yake ya kugombea haijawahi kuyumba na ndio maana mwaka huu amechukua tena fomu hiyo, akiamini ana uwezo, nia, na anazifahamu changamoto za wananchi wa Kigoma Mjini.
“Ninaamini nitapewa ridhaa kwa sababu nina uwezo, dhamira, nia, na natambua changamoto za wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini. Na endapo kura hazitatosha, kama ilivyokuwa mwaka 2020, nitaendelea kushirikiana na wananchi, wanachama, na viongozi wa chama ili kuhakikisha ushindi wa chama,” ameeleza.
Amesisitiza kuwa atahakikisha mgombea atakayepitishwa na chama anashinda kwa kura nyingi na za heshima, ili kurejesha hadhi ya mji wa Kigoma Mjini, kukamilisha miradi ya maendeleo ya 2015–2020, kuboresha uchumi wa wananchi, na kurejesha sauti ya utetezi Bungeni.
“Jimbo la Kigoma Mjini siyo la majaribio, siyo la mizaha wala la kutafutia umaarufu. Ni jimbo la watu waelevu wanaojua wanataka Mbunge wa aina gani. Tumejidhatiti kurejesha hadhi ya mji wetu,” amesema.
Nondo amesisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya kampeni za nguvu, kulinda kura na kupambana dhidi ya hujuma zote za dola na CCM, kuhakikisha ACT-Wazalendo inashinda nafasi ya Ubunge na kurejesha uongozi wa Manispaa ya Kigoma Mjini chini ya chama hicho katika uchaguzi wa 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED