Wataalamu wa mazingira wamesema malengo ya kufanikisha uchumi wa bluu hayatatimia kikamilifu, endapo mazingira ya bahari ambayo ni chanzo cha uchumi huo hayataendelezwa vizuri kwa faida ya sasa na baadaye.
Mkurugenzi wa Transforming life, Naishivai Mollel alisema hayo juzi wakati wa usafishaji fukwe jijini Dar es Salaam, ulioshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wanafunzi wa sekondari.
Usafi huo ulifanyika katika ufukwe wa Daraja la Selander jijini Dar es Salaam ukishirikisha taasisi tatu ambazo ni transforming life, sanamare na mazingira connect na pia shule mbili za sekondari.
Naishivai alisema, mazingira machafu katika bahari ni hatarishi kwa viumbe wa baharini ikiwemo samaki ambao hutegemewa katika uchumi nchini.
"Tumekuja na kampeni hii inaitwa 'beyond the shoreline' kwa kiswahili zaidi ya ufukweni ili kuweka bahari katika hali ya usafi. Uchafu umejaa baharini kuna picha tunazo zinazoonesha samaki amekula kipande cha plastiki sasa hii ni hatari kwa usalama wa viumbe baharini na uchumi wa bluu" alisema Naishivai.
Mratibu wa taasisi ya Sanamare, Pius Silas alisema taka za majumbani ndizo zinazoongoza katika uchafuzi wa bahari na hivyo kampeni hiyo inalenga kujenga tabia ya usafi kwa vijana kwa faida ya sasa na baadae.
Alisema pia wanalenga kufanya utafiti zaidi kujua aina ya taka hizo za majumbani zinazoongoza ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia katika utungaji wa sera za mazingira.
Alisema kampeni hiyo ya uhifadhi mazingira imefanikiwa kuwafikia wanafunzi zaidi ya 7,000 katika wilaya tano za Jiji la Dar es Salaam, huku ikilenga kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
"Tumeona jinsi vijana wanavyoweza kuwa mabalozi wazuri tunajivunia kuona vijana wakiongoza kampeni za usafi na kuelimishana kuhusu madhara ya taka katika bahari na kisha kutumia ubunifu kufikisha ujumbe kwa jamii," alisema Silas.
Mwalimu Janeth Fussi kutoka Shule ya Sekondari Magoza alisema wamekubali kuwashirikisha wanafunzi katika kampeni hiyo ya usafi ili wapate mafunzo kwa vitendo kuhusiana na athari za uchafuzi wa mazingira ya bahari, ili wawe mabalozi wa mazingira kwa wanafunzi wenzao na pia kwa jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED