Wananchi 4,133 wapata huduma za kisheria Sabasaba

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:50 AM Jul 14 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Damas Ndumbaro(mwenye kofia), akitoa huduma ya msaada wa kisheria
Picha: Elizabeth Zaya
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Damas Ndumbaro(mwenye kofia), akitoa huduma ya msaada wa kisheria

WIZARA ya Katiba na Sheria imesema Jumla ya wanananchi 4,133 wametembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwenye maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF) yaliyoanza Juni 28, mwaka huu na kuhitimishwa jana

Na waliopatiwa huduma ya msaada wa kisheria ni 121 na kati ya hao wanaume 64 na wanawake 57.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara hiyo, Beatrice Mtembo, maeneo waliyotoa elimu ni watu kujua haki zao za kikatiba, elimu ya masuala ya ardhi, ndoa, mirathi, kesi za jinai na za madai. 

Kadhalika, amesema wamefanikiwa kutatua migogoro ya papo kwa papo kwa asilimia 80 ambayo waliipokea kwenye maonesho hayo na mingi ikiwa ni kuhusu masuala  ya ardhi, matunzo ya watoto, ndoa na mirathi.

Pia, amesema kupitia maonesho hayo,  wametoa elimu kuhusu vitengo mbalimbali vilivyopo katika Wizara hiyo ikiwamo idara ya haki za binadamu, idara ya huduma za kisheria kwa umma, idara ya katiba na ufuatiliaji haki na kitengo cha uangalizi wa utajiri na maliasili za nchi.

"Na kikubwa zaidi kuanzia Juni 28 tulikuwa tunapimwa na Tantrade ambao ni waandaaji wa maonesho haya na hatimaye kupitia huduma bora ambayo watendaji wa Wizara na wadau wengine ambao tumeshirikiana nao wameitoa, tumekuwa wa kwanza katika Wizara zilizoshiriki katika maonesho haya.

"Hii inathibitisha kwamba huduma zilizokuwa zinatolewa ni bora na wananchi walikuwa wanaridhika kwa huduma waliyoipata,"amesema Beatrice. 

Amesema baada ya maonesho hayo kumalizia huduma za msaada wa kisheria zitaendelea katika ngazi ya halmashauri. 

"Tunawaelewesha wananchi kwamba maonesho yameisha lakini huduma hazijakoma, huduma hizi ni endelevu na zinapatikana katika halmashauri zote za mkoa.

"Hivyo, ile migogoro ambayo tumeibeba sabasaba itaendelea kushughulikiwa na hata ile mipya ambayo haikuletwa sabasaba inapokelewa kwenye halmashauri zote," amesema Beatrice.