Mollel ataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao nje ya nchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:10 PM Jul 14 2025
Mollel ataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao nje ya nchi
Picha:Mpigapicha Wetu
Mollel ataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao nje ya nchi

Wazazi ambao watoto wao wanakwenda kusoma nje ya nchi kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 wametakiwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa watoto wao kitaaluma na tabia.

Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL),  Abdulmalik Mollel alipokutana na wazazi na wanafunzi hao siku ya Jumapili kwenye ofisi za GEL jijini Dar es Salaam ambapo wazazi na wanafunzi hao walipewa taratibu  za mambo ya kuzingatia kabla, wakati na baada ya kufika nchi wanazokwenda.

Katika mkutano huo, ambao ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani, wanafunzi wengi walikabidhiwa viza zao tayari kwa ajili ya safari ya kuelekea vyuoni, huku wazazi wakipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na baadhi ya wawakilishi wa vyuo hivyo.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema wazazi wanalipolipa ada wasidhani kwamba wamemaliza jukumu lao na badala yaake bado wanakuwa na wajibu wa kuwafuatilia.

Alisema ni muhimu sana kila mzazi akafanya hivyo  ili kujua maendeleo ya mtoto wake kitaluma na tabia anapokuwa chuoni kwani baadhi yao wamekuwa wakibadilika na kufanya mambo yasiyostahili na kushindwa kuhitimu.

“Mzazi ukiona mtoto wako ana nyendo ambazo hazieleweki eleweki mwite nchini ukae naye uzungumze naye ujue shida yake kwasababu unaweza kukuta ameshaacha shule anafanyabiashara,” alisema Mollel

“Cha msingi kinachowapeleka kule nje ya nchi ni masomo siyo biashara, mkifika kule na kuanza kufanyabiashara mnaweza kushindwa kuhitimu kwa hiyo wazazi mnapaswa kuwa karibu sana ukiona mtoto wao kila akikupigia simu hana mazungumzo zaidi ya kuomba hela hapo anza kushtuka na kumfuatilia,” alisema


Mollel alisema ataendelea kutekeleza wajibu wake kuhakikisha kila mwanafunzi aliyekamilisha taratibu anafanikisha safari yake ya kwenda kuanza masomo katika vyuo walivyodahiliwa kwa wakati.

Alisisitiza kuwa maslahi ya mwanafunzi ndiyo kipaumbele cha kwanza na kwamba hatakubali kuona chuo chochote kinashindwa kutimiza wajibu wake.

Aidha, Mollel aliwakumbusha wazazi na vyuo husika kuhusu majukumu yao ya msingi katika kuhakikisha mafanikio ya safari ya kielimu ya watoto wao.

Katika mkutano huo, baadhi ya wazazi na wanafunzi waliotoa ushuhuda, wameeleza kufurahishwa na jinsi ambavyo Global Education Link imekuwa msaada mkubwa katika kutimiza ndoto zao.

Frank John alisema kama si kampuni hiyo, watoto wao wangeweza kujikuta  mikononi mwa mawakala wa elimu ambao siyo waaminifu na kuwatapeli.


“Tunashukuru kuona GEL inasimamia kila kitu kuanzia Dar es Salaam hadi mwanafunzi anapofika chuoni na kizuri zaidi ni kwamba hata akifika chuo hawaishii hapo, wanafuatilia maendeleo yake ya kitaaluma kuhakikisha anatimu na kama anachangamoto yoyote wanaitatua,” alisema


Miongoni mwa wanafunzi waliopata nafasi ni wale waliodahiliwa katika chuo cha Dalian Neusoft University of Information (DNUI) cha  China.

Wanafunzi hao wamedahiliwa  kwa programu ya Bachelor of Computer Science  miaka minne na  Bachelor of Engineering in IT .

Hiyo ni moja ya programu bora zinazochanganya masomo ya kompyuta na uhandisi wa teknolojia ya habari.


“Hii ni fursa adhimu ya kielimu inayompa mwanafunzi uzoefu wa kimataifa na kazi kwa vitendo kupitia (Optional Practical Training)  OPT katika kampuni za teknolojia nchini China,” alisema mzazi Emmanuel Mbaso.


Katika tukio hilo, wazazi na wanafunzi walitumia nafasi hiyo kuipongeza Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwa kutoa matokeo na Result Slips kwa wakati.

Mzazi Juma Kassim alisema kutoa matokeo mapema kumewezesha  wanafunzi kukamilisha nyaraka za udahili kwa vyuo vikuu vya kimataifa kwa ufanisi mkubwa.

Mkutano huo ulitumika pia kuyajibu maswali muhimu kutoka kwa wazazi na wanafunzi na wanafunzi wengi  tayari wamekamilisha hatua muhimu kama upatikanaji wa VIS na  muda wowote kuanzia mwezi Agosti, wataanza safari ya kuelekea katika vyuo mbalimbali duniani.