Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika (AUABC) imetaja hatua tano zinapaswa kupewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya rushwa na kusisitiza vitendo vya rushwa vinasababisha madhara makubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwamo kuathiri michakato ya uchaguzi barani Afrika.
Kwa mujibu wa AUABC, hatua hizo ni kuimarisha taasisi za kupambana na rushwa, kuboresha mifumo ya uwajibikaji, kuhamasisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kuwekeza katika elimu na uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa sheria bila upendeleo.
Wakati Bodi hiyo ikitaka hatua hizo, Tanzania imeendelea kupiga hatua kila mwaka katika mapambano ya rushwa kutoka nafasi ya 87 kati ya nchi 180 mwaka 2023 hadi nafasi ya 82 kwa mwaka 2024 kwa nchi zilizofanyiwa utafiti baada ya kupata alama 41.
Akizungumza leo jijini hapa kwenye maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika, Mjumbe wa Bodi hiyo Benjamin Kapera kwa niaba ya Mwenyekiti Kwami Senanu;
Amebainisha madhara mengine ya rushwa ni wagonjwa kushindwa kupata matibabu hospitalini, vijana kukosa haki zao na kudhoofisha mifumo ya utoaji haki.
Amesisitiza umuhimu wa kuchunguza kwa kina madhara yanayotokana na vitendo vya rushwa.
Amesema kwa mujibu wa Mfuko wa Mo Ibrahim, Afrika inapoteza takribani dola za marekani bilioni 128 kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa, sawa na asilimia 50 ya mapato yake ya kodi na asilimia 25 ya pato la Taifa.
Ameeleza kuwa hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kwa haraka kushughulikia tatizo la rushwa kuwa ni kuwezesha taasisi ziwatumikie watu.
“Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa zinapaswa yathamini na kuwatumikia watu, kuhakikisha kwamba haki inapatikana, bila upendeleo, na inapatikana haraka kwa wote, bila kujali hadhi,”amesema.
Pia, amesema ni muhimu kuwekeza katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), zana za kidijitali zinapaswa kutumika kwa sababu zinaweza kufanya serikali iwajibike, kuhakikisha huduma zinatolewa kwa usawa, na kuzipa sauti jamii zilizotengwa.
“Kuwekeza katika elimu na kujenga uelewa, elimu ya kiraia inapaswa kupanuliwa na kutengewa rasilimali za kutosha. Inapaswa kuhamasisha vijana wetu na raia wote kuheshimu sana maadili, uadilifu, utu, usawa, na uongozi wa kimaadili,”amesema.
Amesisitiza watetezi wa haki za binadamu, watoa taarifa za siri, waandishi wa habari, na wanaharakati wanapaswa kulindwa dhidi ya kulipiza kisasi, kwa sababu ujasiri wao unatetea utu wa wote.
Akihutubia kwenye maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema Tanzania inajivunia hatua ilizochukua katika kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kutekeleza mkataba wa Umoja wa Afrika ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Amesema ripoti inayotolewa na Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na mapambano dhidi ya rushwa inaonesha Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano hayo kila mwaka tangu 2019.
“Haya ni mafanikio makubwa katika taifa na yanapaswa kutupa hamasa ya kufanya vizuri zaidi kwa kuwa mafanikio haya yanatokana na michango ya wadau mbalimbali, na lazima tubuni mbinu mpya za kupambana na rushwa, tuendelee kujenga mifumo ya TEHAMA ili kutompa uhuru mtu au kikundi cha watu kufanya maamuzi na kuchochea uwazi,”amesema.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amesema Katiba ya Tanzania inataka serikali na taasisi zake kuhakikisha vitendo vyote vya rushwa na aina zote za dhuluma, ubaguzi, uonevu na upendeleo vinaondolewa nchini.
Hata hivyo, amesema rushwa ni kikwazo kikubwa kinachochangia uwepo wa vitendo vingine vya kidhalimu vinavyokatazwa na Katiba na vinadhalilisha utu wa jamii na kwamba wakijiimarisha kwenye mapambano hayo itasaidia kufikia lengo la serikali la kuleta ustawi wa watanzania.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), Ali Abdalla Ali, amesema rushwa bado inaeleweka kuwa miongoni mwa maadui wanaodumaza maendeleo, kuchochea umaskini na kusababisha watu kukosa huduma za msingi.
Alizikumbusha taasisi zinazoratibu maambano dhidi ya rushwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kulinda utu na haki za kila mtu ili kuimarisha utawala bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED