Wanasiasa nchini wametakiwa kufanya siasa za kistaarabu kwa kuwashawishi wapiga kura kwa hoja badala ya kuvuruga amani iliyopo.
Wito huo umetolewa leo, Julai 11, 2025, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Dodoma, Askofu Evance Chande, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mkoani humo.
Askofu Chande amesema kuwa amani iliyopo nchini ni tunu ya thamani inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote, kwani ikivunjika, huichukua muda mrefu kuirejesha.
“Ndugu zangu Watanzania, sumu haionjwi. Nchi yetu imejengwa kwa misingi ya umoja na mshikamano; hatubaguani kwa misingi ya dini wala kabila, hivyo ni jukumu letu sote kuilinda amani hii,” alisema.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED