Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu ametoa kauli kali dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), akikituhumu kwa kutoonyesha nia yoyote ya kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unakuwa huru na wa kuaminika.
Akizungumza Julai 10, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, Semu alisema, "Chama cha Mapinduzi. Hakitaki kusikia wala hakijafanya jitihada zozote kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na kuaminika."
Aliongeza kuwa chama chake kimejipanga ipasavyo kukabiliana na mazingira yoyote ya kihuni katika uchaguzi. “Sisi tunawaambia kuwa tumejipanga. Tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa na mikakati,” alisisitiza huku akishangiliwa na wafuasi.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mijadala kuhusu mazingira ya uchaguzi na usawa wa kisiasa inaendelea kushika kasi nchini, huku vyama vya upinzani vikilalamikia kubanwa kwa haki za kisiasa na usawa wa uwanja wa kisiasa.
ACT Wazalendo imesisitiza kuwa itaendelea kuhimiza uwazi, haki na demokrasia ya kweli nchini, licha ya vizingiti kutoka kwa taasisi za dola na chama tawala.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED