Wachezaji 9 wa Minfootball kwenda kunolewa Libya

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 06:49 PM Jul 11 2025
news
Picha Shufaa Lyimo
Rais wa Chama cha Minifootball Tanzania Deosdedit Mushi akimkabidhi Kocha wa nidhamu Idd Muhunzi vifaa vya michezo pamoja na tiketi za ndege kwa ajili ya Safari yao hapo kesho. Picha na Shufaa Lyimo.

KIKOSI cha wachezaji tisa wa mchezo wa mpira wa minfootball kinatarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Libya kwa ajili ya kushiriki mafunzo pamoja na kufanya majaribio yatakayoanza Julai 13_22 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo pamoja na tiketi Rais wa Chama cha Minifootball Tanzania (TAMFA) Deosdedit Mushi amesema mafunzo hayo yatashirikisha wachezaji kutoka Mataifa 16.

Amesema lengo ni kuwakutanisha wachezaji mbali mbali wenye vipaji pamoja na kuweka uhusiano mzuri baina ya nchi na nchi vile vile utawasaidia vijana wengi kuonekana kuliko kukaa mitaani. 

“Tunaishukuru Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutokana na ushirikiano wanaotupa naamini hawa wachezaji watakwenda kuiwakilisha vema nchi yetu kupitia mafunzo hayo,” amesema Mushi.

Amesema yatashirikisha wachezaji wenye umri kuanzia miaka 16 na kuandelea na kudai upo tofauti kwa kuwa unachezwa na wachezaji sita badala ya 11, isipokuwa sheria zao zinafanana na zile za mpira wa miguu.

1
Kwa upande wake Balozi wa Chama hicho Othman Adam amesema watakwenda kushindana na si kushiriki kutokana na maandalizi ya muda mrefu waliyoyafanya. 

“Tumefanya maandalizi kwa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha tunakwenda kuiwakilisha vizuri bendera ya Taifa letu tunamshukuru Rais Samia kwa juhudi anazozifanya kwenye sekta mbali mbali za michezo hapa nchini manufaa ambayo tunayaona,” amesema Adam. 

Naye, Alex Peter ambaye amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema wamejipanga vizuri licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwenda kushiriki mafunzo hayo. 

“Kwa upande wetu tumejipanga vizuri kwani Kocha wetu ametupa maelekezo ambayo tukiyatumia tutapata mafanikio,” amesema Peter.