Maombi ya Lissu yametupiliwa mbali

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:08 PM Jul 11 2025
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kwa sababu ameyawasilisha kinyume cha sheria.

Lissu aliwasilisha maombi hayo akitaka Mahakama hiyo iitishe jalada la kesi ya tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo dhidi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ili ilipitie na kuchambue mwenendo wa kesi hiyo wa Juni 2,2025.

Aliwasilisha maombi hayo akipinga kuahirishwa huko akidai kuwa hakukuwa na sababu za msingi za kuahirisha kutokana tu na sababu ya upande wa Jamhuri kuomba ahirisho kwa sababu walikuwa wamewasilisha maombi ya kuomba baaadhi ya mashahidi wao kufichwa.

Lissu aliwasilisha mahakamani hapo sababu sita za mapitio, ambapo jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga lilipinga maombi hayo kwa kuwasilisha pingamizi tatu kwa madai kuwa yaliwasilishwa kinyume cha sheria.

Akitoa uamuzi huo mdogo jana Jaji Elizabeth Mkwizu alisema amepitia kwa makini hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa kulikuwa na upungufu wa sheria katika uwasilishwaji wa maombi hayo.

Jaji Mkwizu alisema amekubaliana na ombi la upande wa Jamhuri kwamba maombi ya Lissu yapo kinyume na Kifungu cha 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa hiyo anayatupilia mbali.

"Mleta maomba anapinga amri ya ahirisho la Juni 2, 2025 kwa mujibu wa Kifungu cha 372 (2) cha CPA ni kwamba amri ya ambayo haiitimishi shauri la msingi halikatiwi rufaa wala kufanyiwa mapitio,"

"Kwa hiyo nakubaliana na upande wa Jamhuri kwamba maombi haya yameletwa kinyume na sheria na ya tupilia mbali, kama mwombaji (Lissu) akipenda anaweza kuleta upya maombi yake," alisema Jaji Mkwizu 

Jaji Mkwizu katika kutoa uamuzi huo, aliegemea sababu ya nne ya maombi ya Lissu ya kutaka Mahakama hiyo iagize jalada na kufanya mapitio ya amri ya kuahirisha shauri iliyotolewa Juni 2, 2025 kwa kutokuwepo sababu za msingi, muhimu na za kueleweka zilizochangia kuahirishwa kwa shauri hilo kinyume na sheria za nchi.

Katika hati ya maombi ya Lissu aliomba Mahakama iagize kufanyiwa mapitio mwenendo wa shauri hilo katika kesi ya jinai namba 8606, ambapo Hakimu alikataa kuamua juu ya ombi lililowasilishwa na wakili wake kwamba upande wa mashtaka ulikuwa unaomba, kwa njia ya maombi ya upande mmoja (ex parte).

Pia, Lissu aliiomba Mahakama iagize kufanyika kwa mapitio na kufuta mwenendo mzima wa Mahakama ya Kisutu ulioendelea Juni 2, 2025.

Ilidaiwa kuwa Aprili 3,2025  jijini Dar es Salaam mshtakiwa Lissu akiwa na lengo la kulangai umma alichapisha taarifa hizo kupitia mtandao wa YouTube ambapo maneno hayo yalisomeka ' Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana , wagombea wa Chadema walienguliwa kwa melekezo ya Rais'. 

Maneno mengine yalisomeka ' Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi, pia alichapisha maneno yaliyosomeka Majaji ni Ma-CCM hawawezi kutenda haki wanapenda wapate teuzi kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa,'