Kesi iliyofunguliwa na Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, imeahirishwa hadi Julai 14, 2025, baada ya kushindwa kuanza kusikilizwa jana kama ilivyopangwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Kanisa hilo liliwasilisha shauri hilo mahakamani likiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa na serikali dhidi ya kuendelea kwa shughuli zake za kidini. Maaskofu takriban 500 walihudhuria mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 13, 2025, kusikiliza maendeleo ya kesi hiyo.
Akizungumza na Nipashe Digital, Wakili wa Kanisa hilo, Peter Kibatala, amesema wamewasilisha kesi namba 13189 ya mwaka 2025 dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Taasisi za Kiraia.
Kwa mujibu wa Kibatala, lengo la kesi hiyo ni kuomba Mahakama kutoa amri ya muda itakayoruhusu kuendelea kwa ibada na shughuli nyingine za kidini hadi rufaa dhidi ya zuio la serikali litakaposikilizwa na kuamuliwa rasmi.
“Kesi hii ilipangwa kuanza kusikilizwa leo, lakini kutokana na mwingiliano wa shughuli mbalimbali za kimahakama, Mahakama imeahirisha hadi Jumatatu ijayo, Julai 14, 2025, ambapo maombi yetu yataanza kusikilizwa pamoja na mambo mengine ya kisheria yanayohusiana na shauri hilo,” alisema Kibatala.
Kanisa hilo linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe. Hivi karibuni, mamlaka za serikali zilisitisha shughuli za kanisa hilo kwa madai kuwa linaendesha shughuli kinyume na masharti ya leseni ya usajili.
Taarifa kutoka kwa mamlaka zinasema baadhi ya shughuli zinazotekelezwa ndani ya kanisa hilo zimeonekana kuwa na mwelekeo wa kisiasa kupita kiasi, hali inayodaiwa kutofautiana na malengo ya awali ya usajili wa taasisi hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED