Rais William Ruto ametangaza rasmi uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hatua hiyo inafuatia uamuzi uliotolewa na majaji watatu uliotupilia mbali ombi la kupinga uteuzi huo ambalo lilihoji uwezo wao.
Tangazo katika Gazeti la serikali namba 9269, ya Julai 10, 2025, Ruto alimteua Erastus Edung Ethekon kuwa Mwenyekiti mpya wa IEBC kwa muhula wa miaka sita.
Katika tangazo tofauti la Gazeti la serikali Namba 9270, pia lililotolewa Julai 10, 2025, Ruto alitaja watu sita kuhudumu kama makamishna wa IEBC kwa kipindi kama hicho cha miaka sita.
Wateule ni Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallah.
Mahakama Kuu ilisema wakati uteuzi wenyewe ulikuwa halali, ilani ya awali ya Gazeti iliyotolewa na Rais ilikuwa imechapishwa kwa kukiuka amri ya mahakama.
Matokeo yake, Notisi ya awali ya Gazeti ilitupiliwa mbali, na kuhitaji kuchapishwa upya kulingana na uamuzi wa mahakama.
Kwa matangazo mapya katika Gazeti rasmi la serikali, Mwenyekiti na Makamishna wanatarajiwa kula kiapo mbele ya Jaji Mkuu, ili kuanza rasmi majukumu yao katika Tume ya Uchaguzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED