Uholanzi yaongoza Kampeni usafi ufukwe wa Coco

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 08:56 AM Jul 10 2025
Uholanzi yaongoza Kampeni usafi ufukwe wa Coco
Picha:Mpigapicha Wetu
Uholanzi yaongoza Kampeni usafi ufukwe wa Coco

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer, amesema kampeni ya usafi wa mazingira katika ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam inalenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kusafisha na kurejeleza taka kwa ajili ya kulinda mazingira na kuimarisha afya za watu.

Balozi  De Boer ametoa  kauli hiyo Julai 9,2025 wakati wa zoezi la usafi lililofanyika Coco Beach kwa kushirikiana na Shirika la Africraft, Doors of Hope Foundation, Klabu ya Vyuo Vikuu, pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Azimio,  wakiwa na kaulimbiu ya “No Waste” (Hakuna Taka).

“Tunaamini hakuna kitu kinachoitwa taka, kila kitu kinaweza kutumika tena, hii ni falsafa ya maisha yetu  kurejeleza taka ni mwanzo wa kitu kipya,” amesema  Balozi Boer.

Amesema  kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi si kazi ya mtu mmoja au serikali pekee, alisema iwapo kila mtu atawajibika kusafisha na kutunza taka anazozalisha, hakutakuwa na haja ya kufanya usafi wa dharura katika fukwe au maeneo ya umma.

“Tunataka jamii ibadilishe mtindo wa maisha, badala ya kutupa vitu ovyo, watu wajenge tabia ya kuzikusanya na kuzipeleka kwenye vituo maalum vya urejelezaji,” ameongeza .

Balozi huyo ameeleza kuwa Coco Beach ina kituo cha kudumu cha kukusanyia taka kinachoendeshwa na Africraft, ambacho kiko wazi mwaka mzima na kinapokea taka zinazoweza kutumika tena.

Mbali na kutoa elimu ya mazingira, Boer amesema  urejelezaji wa taka pia ni fursa ya kiuchumi kwani watu wengi sasa wanajipatia kipato kupitia ukusanyaji na utumiaji upya wa taka.

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Doors of Hope Foundation, Shamim Nyanda, amesema  watoto  wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya utunzaji wa mazingira na mabadiliko chanya katika jamii.

“Tunafurahi kuona watoto wanashiriki kufanya usafi zaidi maeneo ya baharini kwa kuwa bahari hupokea uchafu mwingi  na inategemewa kuendesha maisha yetu ya kila siku tunataka bahari kuwa sehemu salama,” amesema  Nyanda.

Naye Ofisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Uholanzi, Chikulupi Kasaka, amesema  ubalozi huo umekuwa mstari wa mbele katika juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha kituo cha kutunza taka ambacho pia kinatoa elimu juu ya uchakataji na urejelezaji wa taka.

“Tunashirikiana vizuri na serikali kupata vibali vya kushiriki usafi, pia tumeweka banda maalum lenye taarifa zote zinazohusu taka katika eneo hili, lina vitengo mbalimbali vinavyohusu usafi, tumeanza kuona mabadiliko  katika fukwe hii,” amesema  Kasaka.

Ameongeza  kuwa elimu ya mazingira inaanzia kwa mtu binafsi na ndiyo maana wanatoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kuwaandaa kuwa mabalozi wa mazingira watakaosaidia kujenga jamii safi kwa siku zijazo.

Kasaka amesema  zoezi ka usafi , limekusanya mifuko 60 ya taka yenye uzito wa zaidi ya kilo 400 zilikusanywa, ambapo sehemu kubwa ya taka hizo zilikuwa plastiki kama vile chupa za maji, mirija ya juisi, na chupa za bia.