KATIKA Karne iliyoko ya 21, Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), ndio inatawala kuwezesha huduma mbalimbali, pia kurahisisha utendaji kazi.
Imeenda mbali, kuwapo mbadala wa binadamu kwa jina ‘akili mnemba.’ Hiyo inafanyika, huku dunia nayo ikiiwa kama kijiji, katika mawasiliano.
Ndani ya kijiji hicho, Tanzania haijabaki nyuma kwenye suala hilo la TEHAMA, katika nyanja mbalimbali zikiwamo sekta nyeti duniani elimu na afya, ambako huduma zinaendelea kuboreshwa kupitia TEHAMA.
Mfano mmojawapo wa kuimarisha huduma kupitia TEHAMA, ni uzinduzi wa huduma za uzazi kwa kupitia programu ya kidijitali kwa wakunga ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi.
Serikali kwa kushirikiana na ubalozi wa Denmark, imezindua programu hiyo iitwayo 'Safe Delivery App' kumsaidia mzazi kujifungua salama.
Ni uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, ikielezwa mfumo huo wa kidijitali utatumiwa na wakunga kujifunza mbinu bora za utoaji huduma zitakazokuwamo katika programu hiyo na kuwafanya waongeze a weledi katika taaluma yao.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Ziada Sellah, katika uzinduzi wa programu hiyo, anasema imekuja kwa wakati mwaka kwa kuwa itamwezesha mkunga kujifunza akiwa mahali popote kazini au nyumbani, cha muhimu ni kuwa na simu janja.
"Uzinduzi wa programu hii ipo chini ya mradi uitwao “10 Million Safe Birth Initiative”, ikatekelezwa katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam kuanzia mwaka huu hadi 2027," anasema Ziada.
Anafafanua kuwa, iwapo mkunga atakumbana na changamoto kazini, anaweza kufungua programu hiyo na kujifunza hatua sahihi za kuchukua kwa ajili ya kutoa huduma, kwa kuwa elimu yote imo kwenye programu hiyo.
"Kinachotakiwa ni kuwa na simu janja tu, kwani programu hiyo itawaongoza hatua kwa hatua kujua nini cha kufanya wakati wa kutoa huduma.
”Vilevile., tuna makundi ya WhatsApp yanayowaunganisha wakunga kutoka maeneo mbalimbali nchini; kwa mfano, mkunga wa Rufiji anaweza kueleza changamoto yake kwenye kundi hilo na kusaidiwa papo kwa hapo," anasema.
Mkurugenzi huyo anasema, kwenye makundi hayo, pia madaktari na wataalamu wa afya wanashiriki kusaidia katika utoaji suluhisho kwa changamoto zinazoibuka wakati wa kuhudumia.
Ili kufikia wakunga wengi zaidi, anasema Wizara ya Afya, imeweka waratibu wa huduma za afya ya mama na mtoto katika kila halmashauri.
Hiyo ni anasema, ni kupitia wakuu wa huduma za ukunga wa mikoa na halmashauri ili kuendelea kujenga uwezo wa wataalamu hao katika maeneo yao.
"Tanzania tuna mfumo mpya wa uzazi salama ambao kwa sasa uko katika halmashauri 30 kwenye hatua za majaribio,
“Baadaye tutaendelea na awamu ya pili katika halmashauri 110, lengo likiwa ni kuhakikisha wadau muhimu ambao ni jamii wanashirikishwa kikamilifu," anasema.
KUTOKA KWA WADAU
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dk. Beatrice Mwilike, anasema kupitia mradi huo, wao wana wajibu wa kutoa mafunzo ya matumizi ya programu hiyo kwa wakunga, kuwaunganisha kwenye mitandao ya mafunzo na kukuza taaluma yao.
Kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na Tanzania na Maternity Foundation, wakunga wote wanapata mafunzo ya jinsi ya kuboresha huduma yao kwa akina mama na watoto na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi,” anasema Dk. Beatrice
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Afya ya Kimataifa (TTCIH), Edward Amani, anasema kituo hicho kitashughulikia uratibu wa shughuli zote za mradi huo, kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi.
"Tutafuatilia kila kinachotekelezwa katika mradi huu ili fedha zitolewe kwa wakati, kwani uwekezaji huu unasaidia wakunga kutoa huduma salama zitakazookoa maisha ya mama na mtoto," anasema Amani.
Mratibu wa Mradi wa UNFPA, Sunday Rwabangiram anasema mradi huo unatekelezwa katika nchi nane za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
"Lengo letu ni kutaka kufikia mwaka 2030, watoto milioni 10 wanazaliwa salama. Wakunga watawezeshwa kutumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa sahihi na kwa wakati,” anasema Rwabangira.
Balozi wa Denmark nchini, Jesper Kammersgaard, anafafanua kuwa serikali ya nchi yake imetoa msaada wa Sh.bilioni 11 kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kupitia Maternity Foundation kwa kushirikiana na UNFPA na Wizara ya Afya.
"Kwa ujumla ni kwamba, mradi huu utatekelezwa kuanzia mwaka huu hadi 2027 na unatarajiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, sambamba na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)," anasema Balozi Kammersgaard
.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED