Waziri Mkuu aombwa kufika kutatua mgogoro wa ardhi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:45 PM Jul 10 2025
Kamishna wa ardhi msaidizi Idrisa Kayera akionesha majina na saini za wanakikundi hao waliofika kwenye ofisi zake na kupewa elimu ya umiliki wa viwanja kwamba unaanzia kwenye ofisi za Halmashauri sio kwa wenyeviti wa mitaa.
Picha: Christina Haule
Kamishna wa ardhi msaidizi Idrisa Kayera akionesha majina na saini za wanakikundi hao waliofika kwenye ofisi zake na kupewa elimu ya umiliki wa viwanja kwamba unaanzia kwenye ofisi za Halmashauri sio kwa wenyeviti wa mitaa.

KIKUNDI cha wakulima 29 wa kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro wamemuomba Waziri Mkuu Khasimu Majaliwa kufika kwenye mtaa wa Kambi tano kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 9 sasa unaosababisha wananchi kutishiwa Maisha, kubomolewa nyumba na kupokonywa viwanja.

Katibu wa kikundi hicho Andrew Gama alisema jana kuwa wanaamini Waziri Mkuu akifika kwenye maeneo yao anaweza kutatua kero inayowakabiri ambayo wameshapeleka malalamiko kwenye ofisi zote kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata, Wilaya hadi Mkoa jambo ambalo halijapatiwa ufumbuzi mpaka sasa.

Gama alisema wao ni wamiliki wa viwanja katika eneo hilo tangu mwaka 2013 hadi 2018 baada ya kununua kutoka kwa mkulima aitwaye Hamisi Msabaha ambae amefariki dunia mwaka 2024 ambaye naye alirithi kutoka kwa mama Mkwe wake Zainabu Saidi.

Alisema ilipofika mwaka 2018 serikali ilipeleka kampuni ya kupima viwanja iitwayo Kaeco na wananchi kutakiwa kulipa malipo ya awali ya shilingi 50,000 na baadhi ya wananchi walilipa lakini baadae hawakuiona kampuni hiyo kuendeleza zoezi hilo.

Waziri Mkuu aombwa kufika kutatua mgogoro wa ardhi
Mmiliki mwingine wa kiwanja kwenye eneo hilo Mecky Philipo alisema kama serikali ilikuwa na uharaka kutaka kuona maeneo hayo yanamilikiwa kihalali kwa nini isingewashirikisha wakazi wa eneo hilo ili wanunue na kupata hati kamili na wao kuamua kuuza kwa wengine.

Mmiliki wa kiwanja katika eneo hilo Mwanaidi Sadala aliiomba serikali kuu iwasaidie sababu yeye akiwa mfanyabiashara ya kukaanga mihogo amejiwekeza na kupata kiwanja na akaamua kumwaga tofali 2000 lakini wanaodai wamiliki wa eneo wamezitumia bila idhini yake kwa kujengea uzio.

Akiongea kwa njia ya simu Mume wa Tamasha Nchimbi - Salehe Mlangwa alikiri kuutambua mgogoro huo na kudai kuwa tayari walishamaliza wakiwa kwenye kikao cha pamoja ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Musa Kilakala ambapo kuhusu kuchukua baadhi ya vifaa vya ujenzi vya wakulima alikiri kufanya hivyo lakini alisema ni baada ya kufanya makubaliano na malipo kwa baadhi ya wakulima.

Akiongea kwa njia ya simu Sakshia Hope alikiri kuingia kwenye mgogoro huo ingawa yeye alidai hahusiki na masuala ya kuwachukulia watu vifaa vyao vya ujenzi na kwamba anamiliki eneo hilo lenye ukubwa wa viwanja vitatu kihalali.    

Mwenyekiti wa mtaa wa Kambi Tano Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro Eliamini Kimario alisema karibu asilimia 70 ya maeneo ya mtaa huo yamepimwa na wengine kupewa viwanja lakini wapo baadhi ya wakulima hawakuridhika na upimaji na kuendelea kuidai manispaa miaka ya 2009/10.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro Idrisa Kayera alikiri kutambua mgogoro huo na kusema kuwa tayari walishakutana na wakulima hao na kujadili juu ya suala hilo na kufikia tamati kuwa wakulima hao walivamia eneo hilo na walipaswa kuondoka sababu eneo hilo lilishapimwa tangu mwaka 1951 na kuandaliwa hati mwaka 1953 na kuwa chini ya mamlaka ya Mkonge.

Alisema Kampuni ya upimaji ilipata kibali Halmashauri na kuanza upimaji lakini baada ya kazi kupelekwa Halmashauri kwa ajili ya uidhinishaji walibaini eneo hilo tayari lilishapimwa miaka mingi na wananchi hao walirejeshewa maelezo kuwa eneo hilo lilishapimwa.