Rais Dk. Mwinyi aikaribisha Canada kuwekeza zaidi katika utalii na biashara

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:12 PM Jul 10 2025
Rais Dk. Mwinyi aikaribisha Canada kuwekeza zaidi katika utalii  na biashara
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Dk. Mwinyi aikaribisha Canada kuwekeza zaidi katika utalii na biashara

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa sekta ya utalii ni sekta ya kipaumbele kwa Zanzibar, ikichangia takribani asilimia 30 ya pato la Taifa, na kuiomba Serikali ya Canada kuhamasisha wawekezaji wake kuwekeza zaidi katika sekta hiyo pamoja na sekta ya biashara.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo Julai 10, 2025, wakati alipokutana na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, aliyefika kwa mazungumzo katika Ikulu ya Zanzibar.

Amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa jukwaa la pamoja kati ya wafanyabiashara wa Canada na Zanzibar ili kuibua na kutambua fursa mpya za kiuchumi na uwekezaji, huku akiwaalika wawekezaji wa sekta binafsi kutoka Canada kuwekeza Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Mwinyi aliishukuru Serikali ya Canada kwa kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia na kutoa misaada ya maendeleo kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, hususan katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Tanzania inathamini uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizi mbili. Ushirikiano huu umekuwa chachu ya mafanikio na manufaa kwa pande zote,” alisema Dk. Mwinyi.

Rais huyo alieleza kuwa bado kuna fursa nyingi zaidi za ushirikiano wa kiuchumi kati ya Canada na Zanzibar, akitaja sekta kama vile uchumi wa buluu, uvuvi wa bahari kuu, mafuta na gesi, kilimo cha mwani, na biashara kuwa na nafasi kubwa kwa wawekezaji wa kimataifa.

Kwa upande wake, Balozi Emily Burns ameipongeza Zanzibar kwa hatua kubwa inazopiga katika maendeleo ya kiuchumi, hususan katika sekta ya uchumi wa buluu na utalii, na kuahidi kuendeleza mashauriano na ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.