Katibu Mkuu wa Chama Cha Makini Taifa, Ameir Hassan Ameir, amesema endapo atapewa ridhaa na wananchi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao, atahakikisha kila Mzanzibari anapokea mshahara wa shilingi 500,000 za Kitanzania kila mwezi.
Ameir ametoa kauli hiyo leo, Julai 10, 2025, wakati wa kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) visiwani Zanzibar. Kikao hicho kililenga kujadili utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 pamoja na matarajio ya ilani mpya ya mwaka 2025-2030.
Akifafanua kuhusu mpango huo wa mshahara kwa kila mwananchi, Ameir amesema kuwa lengo ni kupunguza umasikini, kupunguza utegemezi, na kutoa fursa zaidi kwa vijana na wanawake kujitegemea kiuchumi.
“Ni wakati sasa wa kujenga Zanzibar yenye heshima, usawa wa kiuchumi na mustakabali bora kwa kila raia, bila kujali hali yao ya sasa,” alisema Ameir.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED