Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amesema kuwa chama hicho kiko tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani katika kuongeza nguvu ya ushindani kwa nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwalimu ametoa kauli hiyo leo, Julai 10, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Darajabovu Madukani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Amesema kuwa lengo la CHAUMMA si kuvuruga wala kudhoofisha nchi, bali ni kuchangia maarifa na kuimarisha misingi madhubuti ya mabadiliko yenye manufaa kwa Wazanzibari, huku akisisitiza kuwa chama hicho hakina nia ya kuwa chokochoko dhidi ya chama tawala.
“Tunataka kuona Zanzibar yenye mshikamano, umoja na ushirikiano wa kweli miongoni mwa wananchi ili kwa pamoja tuweze kushinda dhamira ya mabadiliko,” amesema
Amesisitiza kuwa endapo uchaguzi utafanyika kwa uhuru na haki, CHAUMMA iko tayari kumuunga mkono mshindi halali, lakini haitakubali kuona udhalimu na ukiukwaji wa haki za wapiga kura.
Aidha, Salum Mwalimu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya haki, usawa na kutoegemea upande wowote wa kisiasa, akisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwa kioo cha amani na utulivu hasa katika kipindi cha uchaguzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED