FURAHA ya kila mjamzito ni kujifungua salama na kurejea nyumbani, akiwa na afya njema ameshikilia kichanga mikononi, analakiwa na ndugu, jamaa na marafiki, bila kujali mazingira aliyojifungua.
Hapo hapo, kuna wengi wamekuwa wakipoteza maisha, ama mzazi au kichanga kwa sababu ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya kujifungua na kinachotokea, anajifungua kwa kusaidiwa na wasiokuwa na taaluma ya utabibu.
Wapo waliowahi kujifungua majumbani wakabaki salama, pia baadhi wanapoteza maisha. Hiyo ni sababu kubwa iliyoibua serikali kuingia katika operesheni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi, hasa walioko pembezoni.
Ni jitihada za kuokoa maisha wasiishie kukimbilia kwa waganga wa jadi. Hiyo iko ndani ya kiatu cha cha Mpango wa Maendeleo wa Afya ya msingi (MMAM) uliobuniwa na serikali mwaka 2007 na kuanza kutekelezwa mwaka 2008.
Maudhui ya MMAM, yanaeleza mpangilio wa utoaji huduma za afya kila kijiji au mtaa kuwa na zahanati, kata kuwa na kituo cha afya, wilaya hospitali na mkoa kuwa na hospitali ya rufani.
Aidha, inaelekeza kuhakikisha kila mtu anapata huduma za afya jirani yake, miundombinu ya afya inapaswa kujengwa umbali kilomita tano, kwenye mduara wenye kina kilomita 10.
Shirika la Afya Duniani (WHO), baada ya kushuhudia ongezeko la vifo vya wajawazito kutokana na ugumu kuvifikia vituo vya afya nchini, ilisaidia kutatua changamoto hizo, zikiwamo miundombinu kuwaongezea maarifa wataalamu wa afya kitaifa, hatua inayoendelea hadi sasa kwa uwekezaji wa kiserikali.
Miaka saba ya kutekelezwa sera hiyo inatajwa kusaidia kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi 104 mwaka 2022.
Takwimu inayotafsriwa kama hatua kubwa kulinda afya ya mama na mtoto, pia kuchangia kupunguza vifo hivyo kwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya.
Hizo zinafanyika kwa kuboresha hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati, kuhakikisha huduma za uzazi zinapatikana kirahisi, huku hospitali za wilaya 100 zikijengwa pamoja na zaidi ya vituo vya afya 400, kukiboreshwa kwa vifaa vya kisasa.
WAUGUZI MANISPAA
Ukubwa wa tatizo, vifo vya wajawazito na watoto, hivi sasa vinawaibua wauguzi wa Manispaa ya Kahama kuchukua hatua kuanza kufanya kazi mpaka muda wa ziada kutoka uliopangwa kisheria.
Lengo ni kuwafikia wajawazito wote, wauguzi wakijivuna kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Agness Mkanga, Katibu wa Wauguzi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, anaeleza wanavyowajibika kwa muda wa ziada kwa mafanikio.
Ni hatua inayofanyika kuhakikisha kila mjamzito anayefika kwenye huduma za afya kujifungua, anahudumiwa na kurejea nyumbani na kichanga chake.
Anasema mapambano kukabili vifo hivyo yanaanzia kitengo cha kliniki wanakowafikia wajawazito na kujua maendeleo yao na vichanga tumboni, wakielimishwa ya ziada kuhusu uzazi.
Pia, ni namna ya kuwahakikisha wanajifungulia vituoni, kukitokea tatizo wapate msaada wa kitabibu haraka.
Muuguzi Agness anaeleza, watoa huduma ngazi ya jamii, nao wamekuwa sehemu ya mapambano, wakiwafikia na kuwapatia elimu inayostahili.
Hapo Agness anasisistiza kuwa siku zote wanaojifungua njiani wanafikishwa hospitali haraka kuhudumiwa, ikisaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kiwango kikubwa.
Takwimu wilayani Kahama, zinagusa wajawazito kutoka vifo 376 mwaka 2024 mpaka 88 ambayo ni kushuka kwa theluthi tatu (imepungua asilimia 76.6).
Anafafanua sababu kubwa, ni kushirikiana na kujitolea kufanya kazi muda wa kazi.
Muuguzi Agnes, anataja timu nyingine wanaoshirikiana nao ni madaktar, wamekuwa wakiungana kuelimisha katika vituo vya afya, ikiwa sehemu ya ajenda yao ya kidumu.
Anataja kuanzia mwaka jana, mpaka mwezi Mei mwaka huu, wamepunguza vifo vya wajawazito kufika 88 kutoka 376, huku kukiwapo kifo kimoja cha mtoto, kutoka 21.
“Manispaa hii ina jumla ya wauguzi waliosajiliwa 335 sawa na asilimia 76.5 ya mahitaji; wahudumu wa afya 91 sawa na asilimia 52 (ya mahitaji),” anasema.
Katibu wa Wauguzi anafafanua kwamba, hali sasa katika utendaji wao, kila muuguzi anawahudumia wagonjwa 15 mpaka 25, badala ya wastani wa kuwahudumia wagonjwa sita mpaka nane kwa siku.
Hapo inamaanisha wauguzi wa Kahama, wanahudumia ziada ya wagonjwa kati ya saba na tisa, kuna wakati inafika ziada ya wagonjwa 17 hadi 19 kwa siku.
Katika lugha rahisi, wanajitolea kufanya kazi wastani wa mara mbili hadi tatu ya majukumu yao ya kawaida.
ZAMA HIZO
Miaka 10 iliyopita, vifo vya wajawazito na watoto vinatajwa vilishika kasi Kahama, kwa sababu hakukuwa na mwamko wa kujifungua katika vituo vya afya.
Inaelezwa, jambo la kujifungua likasimamiwa na wasio na taaluma ya kitabibu, wakitumia ‘dawa pori’ za kuongeza uchungu kwa wajawazito.
Sura ya takwimu ya miaka mitano ya kwanza inaonyesha vita vya watendaji afya wa Kahama walivyopambana, kuanzia mwanzo wao, hadi hatua ya sasa:
Mwaka 2015, vifo vya kinamama vilikuwa 16, watoto wachanga 312, watoto chini ya mwaka mmoja walikuwa 461 na vifo vya watoto juu ya umri mwaka mmoja hadi chini ya miaka mitano vilikuwa 840; huku jumla ya vizazi hai vikiwa 11,142.
Mwaka uliofuata 2016, vifo vya kinamama viliongezeka kufika 23, watoto wachanga 463, chini ya mwaka mmoja vilikuwa 121 na chini ya miaka mitano 298, hali kadhalika vizazi hai vilikuwa 12,062.
Juhudi za kupambana na vifo hivyo ziliendeleza jamii na mwaka uliofuata, 2017 vifo vya kinamama vilikuwa 18, wachanga 334, chini ya mwaka mmoja kulikuwapo vifo 213 na watoto chini ya miaka mitano walikuwa 483, kwa vizazi hai vilikuwa 13,047.
Pia, mwaka 2018 vifo vya kinamama vilikuwa 15, watoto wachanga 309, chini ya mwaka mmoja 178 na watoto chini ya miaka mitano walikuwa 236. Vizazi hai vilikuwa 18,360.
Mwaka 2019, mnamo mwezi Januari hadi Oktoba vilikuwa vifo vinane, watoto wachanga 281, chini ya mwaka mmoja vilikuwa vifo 35.
ASIMULIA UZOEFU WAKE
Pendo Daniel ni mkazi wa Nyasubi, Kahama, mzazi wa mapacha watatu, anaeleza mchakato wake namna alivyofika kliniki kipindi chote cha ujauzito wake, kupewa elimu ya kujifungua katika mahali sahihi, pia kutotumia dawa kienyeji pasipo maelekezo ya kidaktari.
Anasimulia kwamba hakujua tumboni alikuwa na mapacha, ila alipojihisi yu mjamzito, elimu aliyoipata ikamsaidia kufika kituo cha afya akahudumiwe.
Pendo anakumbuka huduma za awali aipotinga klinilki zilijumuisha kumkagua afya yake dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU, na mwenza wake.
Anasimulia kila anapofika kliniki, amekuwa akasisitizwa kujifungua katika vituo vya afya, vilevile kifanya maandalizi ya mahitaji ya kujifungua salama mapacha watatu.
Mama huyo anasema, kwa sasa hali yao wanaendelea kukua vema, akinena ingetokea amekosa elimu hiyo angejifungulia nyumbani kama walivyofanya baadhi ya ndugu zake, hali ingemwacha hatarini.
Rai yake sasa anawataka wanawake wenzake kila wanapojihisi dalili za ujauzito, wawahi katika kituo cha afya, kama alivyofanya, wakapate ushauri sahihi wa namna ya kulea ujauzito.
Hiyo anaitaja inaendana na pale wanahisi changamoto, wafike haraka katika vituo vya afya, hali itakayosaidia kuendelea kupunguza vifo vya ujauzito, kufika ngazi ya kuvifuta.
MUUGUZI MKUU MKOA
Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Flora Kajumulla, anasema serikali imeboresha vituo vya kutoa huduma kwa kuweka vifaa tiba na dawa za kutosha.
Anataja ulingo wa changamoto uliopo ni kukabiliwa na upungufu wa wuuguzi, pengo wanaloziba wa kuunda timu ya ushirikiano wao kukabilia vifo vitokavyo na uzazi.
WASIMAMIZI TIBA TAIFA
Dk. Saitore Laizer ni Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, katika uzinduzi wa mafunzo kwa vitendo kwa wakunga kuhusu utoaji huduma za dharura kwa kinamama na watoto wakati wa ujauzito, Kahama, ka ana ufafanuzi.
Anasema, licha ya mafanikio kuonekana, bado asilimia 30 ya wajawazito nchini wanajifungua majumbani.
Mganga Mkuu, anasema wazalishaji tajwa wanabaki sio wenye ujuzi unaohitajika kitabibu, hali inayosababisha kuendelea kuwapo vifo vitokanavyo na uzazi usio salama.
Dk. Laizer, anawaagiza watendaji tiba kufikia mustakabali wa kuikomboa jamii, kwa wakunga wa jadi kutambuliwa na kisha kupewa elimu sahihi ya uzazi, ili watakapopatwa na dharura ya mjamzito wamuelekeze kwenda kituo cha afya.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Tanzania, Ziada Sellah, anasema kuwapo madawati ya huduma kwa wateja yamepunguza malalamiko kwa wateja,
Anataja hadi sasa kuna madawati 136 yameanzishwa, kati yake 28 yapo hospitali za mkoa, 57 wilaya, 36 vituo vya afya na zahanati ziko nane.
Ziada anasema, mpaka wameshawafikia wauguzi na wakunga 5,863 katika mikoa 13 ya Tanzania Bara, wakiwapatia elimu ya kumhudumia mjawazito na mtoto, hali inayosaidia kupunguza vifo vya uzazi.
Sellah anataja kukosekana ujuzi kuwa sababu kubwa ya kuwapo vifo hivyo, hivyo akisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje, imetoa mafunzo kwa wauguzi tajwa, akiwataka kila mmoja kuzingatia alichonolewa kitaalamu, ili ionekane katika huduma zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED