Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekipongeza Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kilichopo Wilaya ya Bagamoyo, kwa kuendelea kuwa kitovu muhimu cha mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu nchini.
Pongezi hizo zilitolewa Julai 9, 2025, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, wakati akizindua mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na utawala bora wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa kwa Maafisa Elimu Kata, katika hafla iliyofanyika chuoni hapo.
Prof. Nombo alisema serikali imefanya maboresho makubwa ya sera mbalimbali za elimu, hivyo ni wajibu wa viongozi wanaopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia ujuzi huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera mpya za elimu kwa lengo la kuinua ubora wa elimu Tanzania.
Kwa mujibu wa Prof. Nombo, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Chuo cha ADEM kimefanikiwa kutoa mafunzo kwa viongozi 89,716 kutoka Tanzania Bara na 1,197 kutoka Zanzibar, hatua inayothibitisha mchango wake mkubwa katika kuimarisha uongozi wa elimu nchini.
Aidha, alieleza kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 16 kwa ajili ya chuo hicho ili kuendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wa elimu ngazi mbalimbali, huku akihimiza kuwepo kwa mpango mkakati wa kushirikiana na kupima ubora wa mafunzo yanayotolewa na taasisi binafsi za elimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha ADEM, Dk. Maulid Maulid, alisema kuwa mafunzo hayo yanayotekelezwa chini ya Mradi wa BOOST ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa kitaifa, na kwa sasa yanafanyika katika zaidi ya mikoa 12 nchini, ambapo maafisa elimu kata 294 kutoka mikoa ya Njombe na Mtwara wanaendelea na mafunzo hayo chuoni hapo.
Naye Afisa Elimu Kata wa Ludewa, Mkoa wa Njombe, Lems Mtitu, alisema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka na yatasaidia kuboresha utendaji kazi wa maafisa elimu, hasa katika kuelewa na kutekeleza mtaala mpya wa elimu wa mwaka 2023.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED