Said Soud: Bila mabadiliko ya tume, hakuna uchaguzi Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:51 PM Jul 10 2025
Mwenyekiti wa chama hicho, Said Soud.
Picha: Rahma Suleiman
Mwenyekiti wa chama hicho, Said Soud.

Kauli maarufu ya "No Reform, No Election" sasa imehamia katika Chama cha Alliance for Accountability and Forward Progress (AAFP), ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Said Soud, amesema kuwa bila kufanyika mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hakutakuwa na uchaguzi wa haki na huru visiwani humo.

Soud ametoa kauli hiyo leo, Juni 10, 2025, katika mahojiano na Nipashe Digital, kufuatia taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu msimamo wake wa kushinikiza mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

No reform, no election – hayo ndiyo mawazo yangu kwa upande wa Zanzibar. Tunahitaji mabadiliko ya Tume ya Uchaguzi kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu,” amesema Soud kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa bila ya mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji ndani ya ZEC, vyama vya siasa vitajikuta vikiwa vinamsindikiza tu Rais wa sasa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kupata ushindi.

Kwa mujibu wa Soud, mabadiliko hayo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unaosimamiwa na ZEC unakuwa huru, haki, na unaowezesha ushindani wa kweli wa kisiasa.

Katika hatua nyingine, akizungumzia mgogoro wa ndani ya chama cha AAFP, Soud amekiri kuwepo kwa mvutano huo na kusema kuwa msajili wa vyama vya siasa pekee ndiye mwenye mamlaka na nafasi ya kusaidia kufikia suluhu ya kudumu.

“Msajili ndiye mlezi wa vyama vya siasa, kwa hiyo suluhisho la mgogoro huu haliwezi kupatikana bila yeye kuhusika,” amesema.