Ryan Kalish atua Tanzania kujenga makazi ya masikini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:27 PM Jul 11 2025
Nyota wa zamani wa Major League Baseball (MLB) ya nchini Marekani, Ryan Kalish.
Picha:Mpigapicha Wetu
Nyota wa zamani wa Major League Baseball (MLB) ya nchini Marekani, Ryan Kalish.

Nyota wa zamani wa Major League Baseball (MLB) ya nchini Marekani, Ryan Kalish, ametua nchini kuwatia moyo Watanzania wanaotoka familia masikini, akipanga kufanya matendo ya huruma kwa kuangalia nyumba za masikini na kuboresha makazi yao, kwa kuzijenga upya ama kuzikarabati.

Mbali na ujenzi wa makazi ya masikini, kwa sasa mchezaji huyo wa zamani wa timu za Boston Red Sox na Chicago Cubs, yuko kwenye mazungumzo na Rais wa New Life Foundation Tanzania, Dk. Glorious Shoo, kuona namna wanavyoweza kuwasaidia watoto wa Tanzania.

Akizungumza jana (Julai 10, 2025) baada ya kuwasili katika Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Ryan Kalish amesema: “Baada ya kustaafu, nilipata njia yangu ya kuchagua hivi sasa, kuja kufanya kazi nje ya nchi; kwa sababu kuna mengi ya kuona, na ya kusaidia nikilinganisha na nchi yangu.”

Ryan Kalish, ameongozana na Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwasisi wa Shirika la Together For Transformation la Congo DRC, Shaban Chani, ambaye ni mkimbizi aliyelelewa nchini Uganda.

Baada ya mapokezi hayo, Rais wa New Life Foundation Tanzania, Dk. Glorious Shoo, amesema mchezaji huyo maarufu, anafanya hayo kwa ajili ya kuhimiza waliobarikiwa kuchukua hatua stahiki kwa jamii yetu na kwa ulimwengu kwa jumla.

“Amefika mahali akaona, hayo yote sio jambo la muhimu kujikusanyia umashuhuri, kujikusanyia umaarufu. Lakini wakati huo huo, ni mambo yanayokuhusu wewe tu, haifurahishi moyo; zaidi ya pale unapoweza kuwafikiria wengine na kwenda kugusa maisha ya watu wengine, huo ndio utajiri wa kweli.

…Utajiri wa kweli, si wingi wa magari tuliyonayo, utajiri wa kweli, si wingi wa nyuma tulizonazo. Utajiri wa kweli si wingi wa nchi tunazotembelea, utajiri wa kweli, ni wewe umeweza kugusa maisha ya wanadamu wengine kwa kiwango gani na kwa ukubwa gani.”


Aidha, Dk. Shoo, alisema raia wa Congo DRC, Shaban Chani, pamoja na mazingira yote magumu aliyopitia; leo badala ya kufikiri kwamba ameshatoka kwenye kambi ya wakimbizi ale raha, ameamua kuwajali watoto yatima.

“Kule Uganda, anagusa maisha ya watoto yatima na waliposikia na kufahamu mambo ambayo New Life Foundation tunafanya, wamekuja tujadili namna tutakavyoweza kushirikiana wote kwa pamoja kugusa maeneo mbalimbali ya nchi za Afrika; na hapa kwetu Tanzania, tayari kuna nyumba wanazozitembelea.

Kwa sababu miongoni mwa mambo wanayofanya ni kuangalia baadhi ya nyumba zile masikini na kutafuta namna ya kuboresha nyumba hizo.”

Kwa mujibu wa Dk. Shoo, wanaendelea kufanya mazungumzo ya namna ambavyo pengine wanaweza kuwasaidia watoto yatima wa Tanzania.

Zaidi ameongeza, “Watakuwa mabalozi wazuri wa mbuga zetu za wanyama (Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro-NCAA), mabalozi wazuri wa utalii; na kama hivi wanakaa hotelini wanalipa fedha za kigeni. Ni watu wanaoweza kutumika sana na serikali yetu kwa kuwa ni watu maarufu duniani.”