Shahidi wa upande wa Jamhuri, Sajenti Yohana (F7331), amedai mbele ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuwa alikabidhiwa kutunza vielelezo mbalimbali vikiwemo magunia tisa ya bangi, gari, sare na kofia za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), pamoja na kitambulisho cha jeshi chenye jina la mshtakiwa Ngamba Ngamba.
Ushahidi huo uliwasilishwa jana mbele ya Jaji Sedekia Kisanya, ambapo shahidi huyo alidai kuwa Desemba 23, 2023 majira ya saa 12:00 asubuhi akiwa katika Kituo cha Polisi Ikwiriri, Rufiji, alipokea vielelezo hivyo kutoka kwa Koplo Shabani.
Sajenti Yohana ameeleza kuwa vielelezo alivyokabidhiwa ni pamoja na gari aina ya Toyota Gaia lenye namba za usajili T708 BQR, rangi ya kijivu, magunia tisa ya bangi, simu mbili za mkononi, kitambulisho cha JWTZ chenye namba E6210 kilichoandikwa jina la Ngamba Ngamba, koti na kofia vya JWTZ.
"Baada ya kupokea vielelezo hivyo, nilivihakiki na kuvithibitisha kuwa viko salama kabla ya kuviingiza kwenye kitabu cha kumbukumbu za vielelezo," amesema.
Ameongeza kuwa Desemba 27, 2023, Koplo Pascal alichukua vielelezo hivyo na kuvipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kisayansi, na siku hiyo hiyo usiku alivirudisha magunia hayo ya bangi yakiwa yamefungwa.
Mahakama ilikubali vielelezo hivyo viingizwe kama ushahidi baada ya shahidi kuviomba, licha ya upande wa utetezi kupinga.
Shahidi mwingine, Mkemia wa Serikali daraja la kwanza, Ernest Prosper, amethibitisha kupokea vielelezo hivyo kutoka kwa Koplo Pascal kwa ajili ya uchunguzi. Alisema magunia hayo tisa yalikuwa na alama A hadi I, na yalikuwa na majani makavu yanayodhaniwa kuwa bangi.
Ernest ameeleza kuwa baada ya uchunguzi wa kisayansi, ilibainika kuwa magunia hayo yalikuwa na bangi yenye uzito wa kilo 168.49. Mahakama ilikubali pia kupokea magunia hayo kama vielelezo licha ya pingamizi la upande wa utetezi, ambalo lilitupiliwa mbali.
Wakati akijibu maswali ya Wakili wa utetezi, Benjamin Mageni, kuhusu matobo yaliyokuwa kwenye viroba vya bangi, shahidi alikiri kuwa matobo hayo hayakuwepo awali lakini hakuyaeleza mahakamani kwa kuwa hakukuulizwa kuhusu hilo katika ushahidi wa awali.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Ngamba Ngamba na Silvanus Sebastian, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 168.49 kinyume na sheria, tukio linalodaiwa kufanyika Desemba 22, 2023 katika eneo la Ikwiriri, Rufiji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED