Moshi yaanza na barabara za njia nne

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:03 PM Jul 14 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha; Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mailisita Wilaya ya Hai hadi Kiborloni katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, inarajia kuanza wakati wowote, baada ya serikali kuthibitisha kupokea Sh.bilioni 488 za kukamilisha mradi huo.

Barabara hiyo ni ile inayotoka Arusha kupitia mpaka wa Holili ulioko Rombo hadi Voi nchini Kenya.

 Jana, Julai 13, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema tayari serikali imeshapata Sh.bilioni 488 za kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne.

"Barabara hii kutoka Mailisita mpaka Kiborloni, itajengwa njia nne; na kutoka Kiborloni mpaka Holili, itapanuliwa ili iweze kupitika kwa njia mbili, huku kukiwa na nafasi ya kutosha pamoja na ya waenda kwa miguu.

 ..Kazi hiyo itaanza wakati wowote, na daraja letu kubwa liko pale Kikafu. Barabara hii mpya haitapita kwenye daraja lile tena. Itapita daraja jingine ambalo linanyooka linatokea kule mbele (Kwa Sadala).

 Zaidi ameongeza,"Barabara ile ya sasa itabaki kama ilivyo, ili huko mbele, ambaye anataka kupita daraja jipya apite na anayetaka barabara ya zamani apite. Kila mmoja ataamua mahali pa kupita."

 Machi 3, 2016,Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli na mwenzake wa Kenya, Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta, waliweka jiwe la msingi katika barabara hiyo itakayounganisha Jiji la Arusha na Mji wa Voi, nchini Kenya.

Barabara hiyo kutoka Arusha hadi Taveta inatarajiwa kurahisisha uchukuzi na kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Ina umbali wa kilomita 234, na ni sehemu ya mradi mkubwa wa barabara inayotoka Arusha na kupitia Holili na Taveta hadi Mwatate.